Wilaya nzima ya Pangani kuunganishiwa na umeme ifikapo 2018


Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo amesema kuwa  Serikali ina mpango wa kusambaza nishati ya umeme katika wilaya nzima ya Pangani na kuifanya kuwa wilaya ya mfano ndani ya kipindi cha  miaka miwili.

Waziri wa Nishati na Madini (kulia) akipokea kero mbalimbali kutoka kwa wananchi wa kijiji cha Mkaramo.

Profesa Muhongo aliyasema hayo alipokuwa akihutubia  katika kijiji cha Mkaramo  kilichopo wilayani Pangani mkoani  Tanga. Profesa Muhongo  yupo mkoani  Tanga kwa ajili ya kukagua miradi ya  usambazaji wa umeme  vijijini inayotekelezwa na  Wakala wa Nishati  Vijijini (REA).

Kabla  ya kuwasili katika kijiji hicho msafara wa Profesa Muhongo  ulisimamishwa na wananchi  wa kijiji cha  Sakura kilichopo wilayani Pangani mkoani  Tanga waliokuwa na mabango wakiomba kupatiwa  umeme  katika kijiji chao.

Akizugumza kwa niaba ya wanakijiji wenzake,  Boga Mbega alisema kuwa kijiji hicho kimekuwa  gizani kwa muda wa miaka mingi  hali inayopelekea uchumi katika kijiji hicho kudumaa.

Aliongeza kuwa kutokana na ukosefu wa umeme  katika kijiji hicho wamekuwa wakifuata huduma za jamii  kama  vile matibabu  na maji katika vijiji  vya mbali na hivyo  kuhisi kama wako kwenye kisiwa cha giza.

Mara baada ya Waziri  Muhongo kuwasili katika kijiji cha Mkaramo na kuanza kuhutubia alisema kuwa kutokana na wilaya ya Pangani  kuwa nyuma  kimaendeleo  kuliko wilaya nyingine  nchini, Serikali imepanga mikakati ya kuhakikisha kuwa wilaya  nzima ya Pangani pamoja na vijiji  vyake  vyote inapata nishati ya umeme ndani ya kipindi cha miaka miwili.

Akielezea malengo  ya kuipa kipaumbele  wilaya ya Pangani kwenye  mpango wa usambazaji wa umeme  vijijini chini ya  Wakala wa Nishati  Vijijini (REA), Profesa Muhongo alieleza kuwa ni  kufuta umasikini kupitia uboreshaji wa huduma za jamii kama shule, zahanati, pamoja na kuzalisha  ajira na kupunguza wimbi la  vijana kukimbilia mjini kutafuta ajira.

Mkuu wa Wilaya ya Pangani, Zainab Abdallah Issa (kushoto) akiwasilisha mahitaji ya umeme katika wilaya ya Pangani.

Alisema katika utekelezaji wa mradi wa REA Awamu ya tatu katika  wilaya ya Pangani, maeneo yatakayopewa kipaumbele cha kwanza ni pamoja na shule, zahanati, vyuo, makanisani na misikitini.

Aliwataka wananchi wa wilaya ya Pangani kujiandaa na mradi huo kwa kubuni fursa mbalimbali kama  vile kuanzisha  vikundi  vidogo  vidogo kwa ajili ya kuanzisha  viwanda,  ukulima na  ufugaji wa kisasa ili kujipatia maendeleo.

Alifafanua kuwa   ni wakati wa wakinamama wa wilaya ya Pangani kuachana na matumizi ya kuni  na kutumia majiko ya umeme na gesi.

Profesa Muhongo aliendelea kusema kuwa miradi ya umeme  haihitaji siasa na kuwataka  wananchi kuweka nguvu zaidi kwenye uchumi kwa kutumia nishati ya umeme badala ya kupoteza muda kwenye siasa.

Naye Mbunge wa Pangani Jumaa Hamidu Aweso (CCM) aliishukuru serikali kwa kuipa kipaumbele  wilaya ya Pangani na kusisitiza kuwa wataanza kufanya  uhamasishaji kwa wananchi wote wa Pangani.

Aliwataka wananchi kuachana na maandamano ya siasa na badala yake waweke nguvu kwenye shughuli za kiuchumi zitakazowapatia maendeleo.

Alisema kuwa  mara baada ya umeme katika wilaya nzima ya  Pangani kupatikana, wawekezaji watajitokeza kuwekeza kwenye viwanda vya korosho na kuongezeka mapato katika halmashauri ya  Pangani.

Imeandaliwa na:
Greyson Mwase,
Afisa Habari,
Wizara ya Nishati na Madini,
5 Barabara ya Samora Machel,
S.L.P 2000,
11474 Dar es Salaam,
Simu: +255-22-2121606/7, Nukushi: +255-22-2121606
Barua Pepe: info@mem.go.tz
Tovuti: mem.go.tz

0 Comments

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ZINAZOHUSIANA