Sambaza:

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh Kassim Majaliwa na Afisa Mtendaji mkuu wa Kampuni ya simu Tanzania TTCL Nd. Waziri Waziri Kindamba, kwa pamoja katika uzinduzi wa huduma za TTCL4G LTE mjini Dodoma mapema mwaka huu.

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezitaka taasisi mbalimbali za umma zinazodaiwa na Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) ziwe zimelipa madeni yao ifikapo Juni 30, mwaka huu.

TTCL inazidai taasisi mbalimbali za umma jumla ya sh. bilioni 11.5 ikiwa ni gharama ya huduma walizozitoa kwa taasisi hizo, hivyo kukwamisha utendaji wa kampuni hiyo.

Ametoa agizo hilo leo (Ijumaa, 10 Februari, 2017) wakati akizindua huduma za simu ya mkononi kwa teknolojia ya 4G LTE ya TTCL mjini Dodoma.

Pia amemtaka Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mnyaa Mbarawa akutane na wadaiwa sugu wote wathibitishe madeni husika na kisha wapange namna ya kulipa.

“Nijuavyo, kila Wizara inatenga bajeti kwa ajili ya ankara za simu, sasa haya malimbikizo yanatoka wapi?. Ni lazima wadaiwa wote walipe madeni yao mara moja,” ameagiza.

Waziri Mkuu ameongeza kuwa “unapokuwa na deni lazima ulipe. Mheshimiwa Waziri simamia hili, na unipe taarifa ya utekelezaji kabla ya Mkutano ujao wa Bunge la Bajeti,”.

Pia Waziri Mkuu alitoa rai kwa Menejimenti na watumishi wa TTCL kwa kuwataka watambue dhamana waliyopewa na waitendee haki kwa kufanya kazi kwa bidii na weledi.

SOMA NA HII:  Selfie yamsababishia Mwanamke kifo….Akifurahia maisha.

“Fanyeni kazi kwa bidii, weledi, uzalendo, maarifa na ubunifu wa hali ya juu. Imarisheni Idara ya Masoko, hamasisheni ubunifu kwenye Kampuni na wapeni nafasi vijana wenye uwezo,”.

“Kama hiki ni kizazi cha T, wacha kizazi hicho kiongoze mapinduzi ya T, muhimu uzalendo, uwezo, dhamira na ubunifu vizingatiwe katika kutoa nafasi hizo,”. amesisitiza.

Pia amewataka viongozi wa TTCL wapitie upya muundo wake na wajiridhishe kama unaendana na ushindani wa kibiashara na dhamira ya Serikali ya kupunguza gharama zisizo za lazima.

Akizungumzia suala la idadi ya watumishi wa Kampuni, Waziri Mkuu ameshauri wajifanyie tathmini wenyewe kujua mahitaji halisi ya watumishi na kufanya maamuzi kwa kuzingatia sheria za nchi.

“Serikali inatarajia TTCL ijiendeshe kwa faida na sio kuja kuiomba Serikali ruzuku, hivyo hamna budi kupunguza gharama za uendeshaji wa kampuni kwa kadiri inavyowezekana,” amesema.

Awali, Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa TTCL, Bw. Waziri Kindamba alisema miongoni mwa changamoto zinazokabili kampuni hiyo ni pamoja na mtaji mdogo.

Pia aliiomba Serikali iwasaidie ili waweze kulipwa madeni yao wanayozidai taasisi mbalimbali za umma kutokana na huduma walizozitoa kwa taasisi hizo.

Hata hivyo Bw. Kindamba ameahidi kwamba watafanya kazi kwa biidi ili kuhakikisha TTCL inaongoza kwa kutoa huduma bora za mawasiliano nchini.

Waziri Mkuu katika uzinduzi

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Ndugai wakiteta jambo kwa pamoja na mbunge wa Chalinze Ridhiwani Kikwete pamoja na wabunge wengine.

 

SOMA NA HII:  Taarifa kutoka TANESCO kuhusu mfumo wa ununuzi wa umeme kwa njia ya LUKU

Sambaza:

Written by Mediahuru

Tunaandika kuhusu sayansi na teknolojia kwa kutumia lugha ya Kiswahili.

Leave a Comment

Kumbuka Ni Muhimu Kuandika Jina Lako