Unafanya muziki wa biashara ila ni lini biashara itakutambua ?


Muziki wa kizazi kipya una historia ndefu kuanzia mwaka 1989 mpaka sasa, mwaka 1993 ndipo ilitoka album ya kwanza kwenye muziki wa kizazi kipya ambayo ilikuwa ni mali ya kwanza Unit. Album hiyo iliitwa Kwanza Unit.

Miaka ya 1995 muziki ulishika hatamu na kuona mafanikio ya wasanii walio wengi. Hata msanii Joseph Mbilinyi a.k.a Mr II Sugu alitoa album yake ya kwanza 1995 na kusambazwa na mzee John Kitime, album hiyo iliitwa “Ni Mimi”.

Wakati huo muziki huu wa kizazi kipya ulikuwa na kundi kubwa la wasanii wa hiphop. Waimbaji walikuwa asilimia chache sana. Miaka ikasogea mpaka miaka ya 2000 hapa tuliona muziki ukiwavuta wengi ambao hawakuwa hata na wazo na muziki.

Wengi wao ni wale ambao walihisi muziki ni uhuni, lakini wakati huo tayari walishapata kuona mafanikio waliyopata baadhi ya wasanii.

Muziki kwenda kimataifa haijaanza leo wala jana ni tangu miaka ya zamani, Msanii kama Mr II sugu  mwaka 1998 alifanya onyesho nchini Sweden ambapo alikuwa jukwaa moja na Oliver Mutukuz huku kundi la X Plastaz Maasai mwaka 2003 waliweza kufanya show nje ya Tanzania “X Plastaz Maasai Hip Hop tour 2003 –UK, Belgium na Holland.

Leo hii imekuwa ni kinyume na vile ambavyo ilikuwa. Watangazaji wengi wa vipindi vinavyohusu muziki wa kizazi kipya wamekuwa wakiaminisha wasikilizaji walio wegi kuwa eti muziki wa hiphop sio muziki wa biashara.

Wamekuwa na kauli zao ambazo zinaonyesha walivyokuwa na ufahamu mdogo kuhusu wanachofanya. Ukitaka utafakari yaliyofanywa nyakati za nyuma na wakongwe walio wengi katika muziki wa kizazi kipya hakika ni mengi hasa katika muziki wa hiphop.

Ndio, wasanii wengi  wa sasa wamebadilika sana na wanaendeshwa na upepo huu wa soko la muziki, upepo unaopewa nguvu na baadhi ya media. Wanafanya muziki uliojaa umagharibi na hauendani kabisa na mazingira ya kwetu.

Maisha wanayoishi, vitu wanavyoimba ni hakika, haviendani kabisa na mazingira halisi ya jamii za kitanzania, Nikki wa Pili amewahi kusema “Kama unataka kufanya biashara ya muziki wasikilize zaidi wateja, kuliko wakosoaji”-  Je ni kweli wasikilizaji wanapenda mfanye muziki mnaoufanya sasa ama media ndiyo zinawaaminisha muziki huu ndiyo unatakiwa?

Suala la wasanii wa sasa kusema wanafanya muziki wa biashara wanakuwa wanakosea, kwa sababu hakuna muziki usiokuwa biashara na kufanikiwa au kutokufanikiwa hakutokani na aina ya mziki (genre), kuna mambo mengi ambayo yapo njee ya muziki, yanahusu sanaa nzima, uchumi na mifumo.

Kinachoendelea hivi sasa ni mtazamo walionao watu wengi ambao hawaijui sanaa ya tanzania kwa mapana na changamoto zake! ni mtazamo unaoashiria kutazama mafanikio kwa mlengo mfinyu. Hakuna aina ya mziki wala sanaa Tanzania imefanikiwa kilichopo ni kuwa wengi mnamitazamo mifupi!

Hatusemi watu wengine wasifanye wanachokifanya ila Kama walikuepo huku mwanzoni halafu wakaona kabisa wanachofanya sasa wamebadilika ni mbaya sana kuendelea kuwaaminisha watu kwamba hiki wanachokifanya ndiyo kile walichokuwa wanakifanya Mwanzo.

Tunakwamisha sanaa zetu kwa kutokujua, na kuendelea kudanganyana, mwisho wa siku kuishia pabaya kwa kushambuliwa na msongo wa mawazo baada ya ulichokuwa unakitarajia kukikosa!

Namaliza kwa mistari ya One The Incredible Kutoka kwenye wimbo wa Kivyovyote Wanataka niache ngumu nibane pua, Ninyoe kiduku ndio niwe msanii wanaemtambua, Ila humu nilipo ndio unaponsikia, Na kama haikushiki, hausiki, haitokusaidia”

0 Comments

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ZINAZOHUSIANA