Uchawi Wasababisha Vituo vya Redio 23 Kufungiwa


Tume ya mawasiliano nchini Uganda, UCC, imevifungia vituo 23 vya redio. Vituo hivyo vinatuhumiwa kutangaza uganga wa kienyeji na kuwatapeli wananchi.

Kwa mujibu wa msemaji wa Tume hiyo, Ms Pamela Ankunda, vituo vya redio vilivyofungiwa vimekuwa vikishiriki katika kuendeleza na kutangaza maudhui ya uchawi, huku wakiwaambia wananchi kutuma fedha kupitia njia ya simu za mikononi.

Maamuzi hayo yamefatia baada ya kutolewa onyo kuwa vituo hivyo viache kufanya vipindi na waganga wa kienyeji. Tangazo hilo la kufungiwa vituo vya redio 23 limetolewa jana jioni na mwenyekiti wa Tume ya Mawasiliano Godfrey Mutabazi.

Mutabazi ameshutumu redio hizo kutumiwa na waganga wa kienyeji kuwatapeli wananchi na kuvunja sheria ya uchawi ya kifungu cha pili.

Vituo hivyo vya redio ni: Metro FM, Nile FM, Kagadi Broadcasting Services, Emambya FM, Village Club FM, Radio Kitara, Packwach FM na Tropical FM.

Nyingine ni Apex FM, Bamboo FM, Ssebo FM, Eastern Voice FM, Eye FM, Victoria FM, RFM, Kiira FM, Tiger FM, Greater African Radio, Dana FM, Gold FM, Hits FM na Radio 5.

Redio hizo zitaruhusiwa kurudi hewa iwapo vitakubali kuacha kutangaza maudhui yoyote yanayohusishwa na uchawi au kutojihusisha katika shughuli yoyote ya waganga wa kienyeji.

0 Comments

Your email address will not be published. Required fields are marked *