TP MAZEMBE KUMWACHIA SAMMATA

Tajiri na mmiliki wa TP Mazembe, Moise Katumbi, amemkubalia Mbwana Samatta kujiunga na KRC Genk ya Ligi Kuu ya...

1 0
1 0

Tajiri na mmiliki wa TP Mazembe, Moise Katumbi, amemkubalia Mbwana Samatta kujiunga na KRC Genk ya Ligi Kuu ya Ubelgiji, imefahamika.

Samatta alitarajiwa kurejea Dar es Salaam jana ili ajiandae kwa safari ya Ubelgiji kuanza maisha mapya ya soka barani Ulaya.
Nipashe inafahamu kwamba Samatta tayari ameshasaini mkataba wa awali na Genk wa miaka minne na nusu na sasa anakwenda kukamilisha dili hilo.
Meneja wa Samatta, Jamal Kisongo, alisema jana kuwa Katumbi ameridhia Samatta kujiunga na klabu anayoipenda.
“Samatta aliondoka nchini kwenda Lubumbashi kwa jambo moja kati ya mawili — kuruhusiwa kwenda Genk, au kubaki amalize mkataba wake na Mazembe ili aondoke kwenye klabu hiyo akiwa ni mchezaji huru Aprili,” Kisongo alisema.
“Sasa imekuwa bahati nzuri, Katumbi ameelewa somo na kumkubalia kijana kwenda klabu anayopenda,”alisema.
Samatta aliondoka Dar es Salaam Januari 20, akiwa amefuatana na mmoja wa maofisa wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwenda Lubumbashi, DR Congo kumshawishi Katumbi akubali ofa ya Genk.
Katumbi alikuwa anataka Samatta ajiunge na klabu ya Nantes ya Ufaransa, ambao walikuwa tayari kuilipa Mazembe Euro milioni 1 na kuipa asilimia 25 ya mgawo iwapo watamuuza klabu nyingine mchezaji huyo.
Genk wako tayari kutoa Euro 800,000 kumnunua Samatta kutoka Mazembe na asilimia 20 ya ngawo iwapo itamuuza Samatta klabu nyingine.
Nipashe inafahamu kuwa tayari Samatta (24) amepatiwa viza na Ubalozi wa Ubelgiji kwenda kuanza maisha mapya KRC Genk.
Samatta, Mchezaji Bora wa Afrika 2015, alijiunga na TP Mazembe mwaka 2011 akitokea Simba aliyoichezea kwa nusu msimu, akitokea African Lyon. Ametupia mara 60 katika mechi 103 alizocheza kwenye kikosi cha timu hiyo ya DR Congo.
In this article

Join the Conversation