Nyingine

Simba yapokonywa pointi 3 na TFF

Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) limetangaza kuipokonya Simba pointi tatu na mabao matatu ambazo ilipewa kutokana na mchezo wao dhidi ya Kagera Sugar.

Simba SC ilipoteza mchezo dhidi ya Kagera kwa kufungwa mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera katika Ligi Kuu ya Bara lakini baadaye ilikata rufaa ikipinga Kagera kumtumia mchezaji Mohamed Fakhi ikidai alikuwa na kadi tatu za njano, ndipo ikapewa ushindi huo kupitia Kamati ya Saa 72.

Mara baada ya kamati hiyo kuipa Simba pointi Kagera ikaomba kupitiwa upya kwa suala hilo na ndipo TFF ikatangaza kuwa suala hilo sasa litakuwa chini ya Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF ambayo ndiyo imetoa maamuzi hayo.

Akizungumza na waandishi wa habari juu ya uamuzi huo, Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa amesema kuwa kuna sababu kadhaa zimechangia kuchukuliwa kwa maamuzi hayo ambapo alizitaja kuwa ni:

“Malalamiko ya Simba hayakuwasilishwa kwa wakati muafaka tangu mchezo ulipochezwa, malalamiko yao hayakuwa katika njia ya maandishi, rufaa ya Simba haikulipiwa ada, kikao cha Kamati ya Saa 72 kilikosa uhalali kutokana na kuwashirikisha watu ambao hawana uhalali wa kuwa kwenye kikao.

“Kutokana na sababu hizo kamati imeamua kutengua maamuzi yaliyochukuliwa na Kamati ya Saa 72 na kurejesha matokeo kama yalivyokuwa, pia kamati imemuagiza katibu mkuu wa TFF kuwapeleka baadhi ya wajumbe wa bodi ya ligi katika Kamati ya Maadili ya TFF kwa kosa la kwenda kinyume na kazi zao,” alisema Mwesigwa.

SOMA NA HII:  Idara ya Habari (MAELEZO) Yapokea Msaada wa Vifaa Kutoka Ubalozi wa China

Zinazohusiana

TOA MAONI

Kumbuka Ni Muhimu Kuandika Jina Lako