Nyingine

Sasa Muziki Unajinyonga na kamba yake

Ni nini kimeukuta muziki? Je, muziki wa kizazi cha sasa una nguvu ya kudumu kwa vizazi vijavyo ?

Bendi na wasanii wa zamani bado wanajaza kumbi za starehe na nyimbo zao zinasikilizwa na kupendwa mpaka leo japo zilitoka miongo kadhaa iliyopita.

Hakuna ubaya wa kufurahia muziki wa zamani, lakini ni  muziki gani kizazi chetu kitahusishwa nao na kujivunia ?

Jaribu kusikiliza redio ama angalia Tv, je wanamuziki wa siku hizi watakuwa na nguvu/athari ya kudumu katika jamii zetu kama ilivyo kwa wanamuziki wa zamani?

Ukiangalia Chat za muziki wa bongo fleva utakuta na wasanii kama Shilole, Snura, Navy Kenzo, Bill Nass, Wasafi, Ommy Dimpoz, Nay wa Mitego, Madee, Msami Baby, Chemical, Weusi, Country Boy na Dogo Janja.

Je, unaweza kufikiria utawaambia nini watoto wako kuhusu wasanii hao hapo juu walivyokuwa na nguvu/matokeo mazuri kwa jamii yetu?

Muziki siku hizi unaonekana kama ni kwajili ya hapa tulipo sasa tu, kuliko kuwa na athari ya kudumu kwa jamii kama ilivyokuwa kwa wasanii wa zamani.

Nguvu ya fedha inaupeleka muziki sehemu mbaya. Wadau, baadhi ya vyombo vya habari na kampuni zingine zinazojihusisha na muziki zinashawishi wasanii kufanya vitu ambavyo kwa upande wangu naona vinawapeleka wasanii katika njia isiyo sahihi kabisa.

Kwa mgongo wa kufanya muziki kama biashara ili kupata faida kubwa japo sio wote wanapata faida, imepelekea wanamuziki kutoa nyimbo zisizo ishi na wala haziendani na mazingira ya jamii zetu.

Ndio, baadhi ya wasanii wa siku hizi wanafanya muziki mzuri, kama Nikki Mbishi, Maua sama, Grace Matata, Barnaba, Nash Mc, Diamond na wengineo, Swali ni je wanamuziki hawa wa siku hizi wataingia kwenye historia na kuonekana ni legends ?

Ni nini kimetokea kwa bendi na wasanii waliokua wanafanya muziki mzuri ?

Ndio baadhi ya wanamuziki wakongwe bado wanafanya matamasha na kutoa albums lakini wengi wao si sehemu ya kizazi chetu.

Je Rayvanny anaweza kuingia kwenye historia kama mwanamuziki bora wa kizazi chetu?

Bendi na wasanii wa zamani walikuwa wanazungumzia vitu muhimu na kuongelea  mada zenye ushawishi mkubwa katika muziki wao.

Fikiria kuhusu Profesa Jay. Nyimbo zake sio nzuri tu bali zina kitu cha kujifunza ndani yake.

Profesa Jay aliimba vitu vyenye ujumbe na maana kubwa ndani yake.

Mfano, Kwenye wimbo wa “Msinitenge” hii ni baadhi ya mistari ya yake:

“Baada tu ya kupima nikangundua sio mzima, na sasa nina jukumu la kuokoa jamii nzima, hakuna asiyetambua gonjwa hili ni la hatari, nilichofanya ndugu zangu niliwapasha habari, wengi walinitazama kwa macho ya chini chini, eti kwa kuwa nina upiungufu wa kinga mwilini, na kila mwathirika wanasema amefanya ngono, na hii ndosababu imefanya nifungue mdomo”

Unaupa nafasi gani muziki “unaovuma” kwa sasa ? Fananisha Profesa Jay na kipaji bora cha sasa Rayvanny kwa mistari kama hii kwenye wimbo wake wa “kijuso”:

“Unaringa una nini kijuso, Vijimeno kama Jini Gaucho, Kwani nawe una nini Kituko, Uso na kazi mjini Upo upo, Punguza kelele ooh kelele acha kelele mama kelele, Punguza kelele baba kelele acha kelele bwana kelele”

Wasafi wanatengeneza midundo yenye ladha na wana mitindo mizuri sana, lakini je, kuna maana gani katika muziki wao? Kuna ujumbe gani kwenye nyimbo za Rayvanny, Dogo Janja ama Ney wa Mitego?

Kwa ajili ya kizazi chetu, hebu tuwe na matumaini kwamba wasanii wetu watarudisha mizizi ya muziki kwa kufanya muziki kwa  dhati ya moyo na kufanya Tanzania kuwa mahali bora, sio kuiharibu zaidi .

Kutengeneza muziki si swala la kupata pesa tu, ila ni kuhusu kuibadilisha jamii kuwa bora zaidi.

Je, kuna wakati zitatokea harakati zingine katika muziki kama Hali Halisi na Okoa Hip Hop?

Je, kuna aina mpya ya muziki itatokea na kufanya watu wasahau kabisa muziki wa zamani?

Je, kuna msanii mwingine atakuja kubadilisha kabisa huu muziki kama Profesa Jay na wanzake walivyofanya miaka ya 1990?

Angalia chat mbalimbali za muziki kwa sasa ,ni ngumu kupata msanii ambaye bado atakuwa bora miaka mitano ama sita ijayo.

Je, muziki wa sasa utasimama imara na kuleta mabadiliko?

Tujipe matumaini kwamba siku moja tunaweza kuja kuwaambia watoto wetu kwamba sisi tumekua kipindi ambacho muziki bado ulikua unaweza kuleta mabadiliko kwa jamii na kuifanya iwe bora zaidi.

 

Soma na hizi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Close