Nyingine

Ripoti ya uvamizi Clouds : Makonda alitishia kuwaingiza kwenye skendo ya dawa za kulevya

Hatimaye kamati maalum iliyoundwa na waziri wa habari, utamaduni, sanaa na michezo, Nape Nnauye kuhusu tukio la mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuzivamilia studio za Clouds Media Group, Ijumaa iliyopita akiwa na askari wenye silaha nzito, imekabidhi ripoti yake.

 

Kamati hiyo iliyoundwa na watu mbalimbali akiwemo mhariri mtendaji wa New Habari Corporation, Deodatus Balile, imethibitisha kuwa ni kweli Makonda alienda katika kituo hicho usiku wa Ijumaa akiwa na askari na kuwashinikiza watangazaji wa kipindi cha Da W’keend Chat show (Shilawadu) warushe kile alichokiita kipindi chake na baada ya kugoma aliwatishia mambo kadhaa.


Kamati hiyo imesema moja ya vitisho hivyo ni kuwakagua watangazaji hao kama wanahusika na uuzaji wa madawa ya kulevya ‘ama kuwabana wadhamini wa kipindi hicho na pengine kuwaingiza kwenye orodha ya kuuza dawa za kulevya.’

Imedai kuwa watangazaji wa kipindi hicho walipatwa na taharuki kubwa kiasi cha kujikuta wakilia na kushindwa kufunga kipindi chao. Imesema mkuu huyo wa mkoa alitumia takriban saa nzima katika kituo hicho na kuwataka wafanyakazi wake kuwa yaliyotokea yabaki ndani ya siku hizo.

Kamati hiyo imesema tukio hilo limeingilia uhuru wa uhariri na uvunjifu wa amani kutokana na vitisho alivyovitoa mkuu huyo wa mkoa. Pia kamati imekiri kuwa Makonda alikuwa ‘mgeni mwenyeji’ kwenye kituo hicho na March 14 alikaaa katika ofisi hizo hadi saa 10 alfajiri kuhariri na watayarishaji kipindi maalum cha kuadhimisha mwaka mmoja wa uongozi wake.

SOMA NA HII:  Teknolojia 5 Maarufu kwenye Magari Kwa Sasa

Hata hivyo wafanyakazi wa kituo hicho wamedai kuwa mkuu huyo wa mkoa hakuwahi kwenda na askari wenye silaha katika siku zingine kabla ya March 17. Pia imedai kuwa hakuna mtangazaji aliyepigwa wala kuumizwa kwenye tukio hilo.

Mapendekezo ya kamati hiyo ni:

1. Mkuu wa mkoa aombe radhi Clouds na kwa wanahabari wote

2. Waziri husika atoe taarifa kwa mamlaka husika ili Mkuu wa Mkoa achukuliwe hatua

3. Vyombo vya usalama kufanya uchunguzi juu ya askari kuingia Clouds na silaha za moto

4. Kampuni ya Clouds ipitie upya kanuni, miongoni na sheria za utangazaji ili kuwa na udhibidi wa watu kuzoea kuingia mara kwa mara pasipo kuwa na taaluma ya habari

Zinazohusiana

TOA MAONI

Kumbuka Ni Muhimu Kuandika Jina Lako