Nyingine

Polisi yaongoza kuwa na watumishi hewa na madeni makubwa

Katika ripoti hiyo iliyowasilishwa bungeni mjini hapa juzi, CAG Assad anasema kuwa mbali na Polisi, taasisi nyingine 18 ikiwamo Mahakama na Wizara ya Maji na Umwagiliaji zimelipa fedha kwa watumishi hewa na kuisababishia serikali hasara ya mamilioni ya shilingi.

Katika kitabu chake cha ukaguzi wa hesabu za Serikali Kuu, CAG Assad anasema amebaini taasisi 19 zililipa kiasi cha Sh. bilioni 1.4 kama mishahara kwa watumishi 260 walioacha kazi, kufa, kustaafu na kufukuzwa.

Anasema mishahara hiyo ililipwa kwa kipindi kati ya mwezi mmoja hadi 72, kinyume na Kanuni ya 113 ya Kanuni za Fedha za Umma za Mwaka 2001 inayosema maofisa masuuli watunze nyaraka za watumishi ili watumishi wanaolipwa wawe ni wale waliokuwapo na kufanya kazi.

SOMA NA HII:  Bomba la usafirishaji gesi asilia kati ya Mtwara na Dar es salaam lina udhaifu mkubwa

Hata hivyo, katika ripoti hiyo, Prof. Assad anasema hadi kufikia Januari 2017, kiasi cha Sh. 158,350,788 kilikuwa kimesharejeshwa.

Katika mchanganuo wake, CAG anasema Jeshi la Polisi lilipa Sh. milioni 757.316 kwa watumishi hewa 139 huku likirejesha Sh. milioni 14.035, Mahakama ililipa Sh. milioni 182.913 kwa watumishi hewa 27 na kurejesha Sh. milioni 35.032 huku Wizara ya Maji na Umwagiliaji ikirejesha Sh. milioni 47.04 kati ya Sh. milioni 63.325 ilizozilipa kwa watumishi hewa 26.

Taasisi nyingine kwa mujibu wa ripoti hiyo ya CAG ni pamoja na Sekretarieti ya Mkoa – Kigoma iliyolipa Sh. milioni 150.228 kwa watumishi hewa 12, Wizara ya Elimu watumishi nane, Wizara ya Afya (8), Wizara ya Ujenzi (4), Idara ya Zimamoto (4), Bunge (2) na Msajili wa Vyama vya Siasa mtumishi mmoja aliyelipwa Sh. milioni 22.443.

Machi 12, mwaka jana, serikali ilitangaza kusitisha ajira na kupandishwa madaraja ya mishahara kwa watumishi wa umma ili kupisha uhakiki wa watumishi hewa na vyeti vya kitaaluma na kitaalamu vya watumishi wote wa umma, uhakiki ambao umefanyika kwa mwaka na siku 19 kabla ya kuhitimishwa rasmi Machi 31, mwaka huu.

Aidha, ripoti ya CAG imeonyesha kuwa Polisi pia imeongoza kwenye orodha ya taasisi za serikali zenye madeni makubwa yanayofikia jumla ya Sh. trilioni 1.979.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya CAG, hadi kufikia Juni 30, 2015, taasisi 92 zilikuwa na madeni kiasi cha Sh. 1,979,323,563,821, ikiwa ni ongezeko la Sh. bilioni 536.155 (asilimia 37) kulinganishwa na mwaka uliotangulia.

“Sehemu kubwa ya deni inatoka Jeshi la Polisi ambalo lina deni la Sh. bilioni 730, sawa na asilimia 37 ya jumla ya deni lote, ya pili ni Wizara ya Ujenzi (Sh. bilioni 271) ikiwa na asilimia 14 ya jumla ya deni ikifuatiwa na Wizara ya Afya (Sh. bilioni 259) ikiwa na asilimia 13 ya jumla ya deni lote,” anasema CAG Assad.

Katika ripoti yake ya mwaka 2014/15, CAG alibainisha kuwa Polisi ilikuwa miongoni mwa taasisi mbili za serikali pamoja na Shirika la Umeme (Tanesco) zilizokuwa zinatisha kwa madeni.

SOMA NA HII:  Mkataba wa Mlimani City na Chuo Kikuu cha UDSM ni wizi mtupu

Zinazohusiana

TOA MAONI

Kumbuka Ni Muhimu Kuandika Jina Lako