Uchambuzi

Namna ya kuifanya simu yako idumu na chaji muda mrefu

on

Ujio wa matumizi ya simu za kisasa maarufu kwa jina la Smartphone umewafanya Watanzania wengi kuzinunua, kutokana na kuwa na uwezo mkubwa wa mawasiliano.

simu

Simu hizi ni sawa na kuwa na kompyuta ya kawaida iliyounganishwa na mtandao wa intaneti.

Kwa mfano, simu hizi zinakupa nafasi kubwa ya mawasiliano kupitia mitandao ya kijamii ya WhatsApp, Facebook, Skype, Viber, Kik Messenger, Twetter, WeChat, LinkedIn, Badoo, Instagram na Twoo.

Pia simu za kisasa zina huduma mbalimbali zikiwamo za kujua jiografia ya maeneo, vipimo vya joto, mapigo ya moyo, upigaji wa picha na huduma nyinginezo.

Kwa kutumia mitandao ya kijamii watu sasa hawana sababu ya kujisika wapweke, kwani hata ukiwa chumbani peke yako unaweza kuungana na watu duniani kwa kujadili na kupokea taarifa mbalimbali.

Hivyo simu hizi zimeweza kuwakusanya watu waliotawanyika sehemu mbalimbali na kujadili mambo kama vile wamekusanyika eneo moja.

SOMA NA HII:  Ifahamu simu ya Tecno Camon CX Air bei na Sifa zake

Mbali na hilo, simu nyingi zina uwezo mkubwa wa kasi ya mawasiliano ya intaneti, hivyo kuwa rahisi kutuma na kupokea barua pepe na kupata taarifa kutoka tovuti mbalimbali duniani.

Ni kutokana na mambo hayo, simu hizi zimeonekana ndizo za kisasa na watu wengi wameamua hata kujinyima ili kuzinunua.

Kasoro ya simu hizi

Pamoja na watu wengi kuzipenda, simu hizi zimekuwa ni kero kutokana na uwezo mdogo wa betri zake kudumu na chaji au nguvu za kuziendesha. Awali watu wengi walipenda simu zinazodumu na chaji muda mrefu.

Simu za kisasa zina udhaifu wa kushindwa kudumu na chaji. Nyingi zinatumika kwa saa sita hadi 12. Kwa sababu hii watumiaji wengi wameamua kununua vifaa vya kuhifadhia umeme kwa ajili ya kuzichaji. Vifaa hivi vinajulikana kwa jina la’ power banking’

Kinachokuonyesha kuwa uwezo unapungua ni pale unapojikuta siku za mwanzo unachaji kwa siku moja baadae mara mbili kwa siku, mara tatu na hatimaye unajikuta unachaji mara kwa mara.

Kwanini simu hizi hazidumu na chaji kwa muda mrefu kama zilivyo simu nyingine? Nini kifanyike ili kutatua tatizo hili? Wataalamu wana majibu.

Sababu za kuisha chaji mapema

Mmoja wa waanzilishi wa Kampuni ya Farbe Tecnik inayojihusisha na utengenezaji wa vifaa vya kuchaji simu, Shane Broesky anasema kupungua kwa uwezo wa kuhifadhi chaji kwa simu hizi ni uzembe wa watumiaji.

Anasema watu wengi hudhani kuziacha simu zao zikiwa zinachajiwa usiku mzima au kwa muda mrefu ni kupunguza uwezo wa betri kuhifadhi umeme.

Broesky, katika maelezo yake aliyoyatoa kupitia mtandao wa Digital Trends, anawatoa hofu wamiliki wa simu kuwa kuziacha kwenye chaji kwa muda mrefu hakuharibu simu zao.

Anafafanua kuwa hii ni kwa sababu simu hizo zina mfumo mzuri wa kuzuia umeme usiendelee kuichaji betri baada ya kufikia kiwango cha juu cha asilimia 100.

Broesky anasema hii inasaidia kuepusha betri kuchajiwa kupita kiasi. Lakini akasema kitendo cha kuicha kwenye mfumo wa kuchaji, kinasababisha kila betri ikipungua kidogo kutoka kiwango cha juu, ianze kuchajiwa tena.

Kitendo hicho kinapojirudiarudia, anasema ndiko kunakoua uwezo wa betri hasa zile za aina ya ‘Lithium-ion’ katika kuhifadhi umeme.

Anasema betri hizi zinapokuwa na kiwango cha juu cha umeme, ikichajiwa joto lake linapanda.

“Kitendo cha betri kuwa kwenye hali ya joto kwa muda, ndiko kunakoharibu uwezo wake wa kudumu na umeme kwa muda mrefu,’’ anasema.

Namna ya kuwezesha chaji kudumu

Ili betri ya simu yako iendelee kuwa na uwezo, Broesky anasema unapaswa uichaji kwa kiwango cha kati ya asilimia 50 na 80. Ukitumia mfumo huo, utaifanya betri ya simu yako iendelee kuwa na uwezo wa juu wa kudumu na umeme kwa muda mrefu.

Jambo lingine la kuifanya betri yako idumu na umeme ni kuepuka betri yako kupungua umeme hadi simu kuzima.

Kampuni ya Simu ya Tecno nayo ilitoa taarifa kwenye mtandao wake kuwa mtumiaji wa simu za kisasa anapaswa kuepuka simu yake kupata moto wakati wa matumizi.

Taarifa ya kampuni hiyo ambayo simu zake zinaonekana kutamba katika soko hapa nchini, inaelezea kuwa iwapo unatumia intaneti katika mazingira ya mawasiliano hafifu, simu hupata moto.

Inawashauri watumiaji wa simu hizo pia wasiziache zikiwa zimefunguliwa ukurasa wa mawasiliano ya intaneti kwa sababu wakati mawasiliano yanakuwa madogo, hupata moto.

About Mediahuru Team

Hapa Mediahuru, tunaandika kuhusu sayansi na teknolojia kwa kutumia lugha ya Kiswahili. Tumejikita kuhakikisha hupitwi na habari yoyote ya teknolojia, endelea kuwa nasi kila siku. - MediahuruDotCom | info@mediahuru.com

Recommended for you

Leave a Reply

Your email address will not be published.