Habari za Teknolojia

Mwongozo wa matumizi bora, sahihi na salama ya vifaa na mifumo ya TEHAMA serikalini

Serikali kupitia Waraka wa Utumishi Na. 5 wa Mwaka 2009 ilitoa maelekezo kuhusu matumizi bora na salama ya vifaa na mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) serikalini. Maelekezo hayo yalitolewa kutokana na kasi kubwa ya ukuaji wa TEHAMA duniani ambayo imesababisha mabadiliko ya uendeshaji wa shughuli za Serikali na jamii kwa jumla na pia kwa kuzingatia kwamba dhana ya TEHAMA ndani ya Serikali bado ni mpya wakati matumizi yake yamekuwa yakiongezeka kwa kasi kubwa. Aidha, ili kujenga misingi imara ya matumizi ya TEHAMA ni dhahiri kwamba waraka huo unatoa dira na mwelekeo thabiti kwa Taasisi na Watumishi wa Umma katika kuwekeza na kuitumia ipasavyo mifumo hii ya TEHAMA ili kuongeza ufanisi na tija serikalini.

Hata hivyo utekelezaji wa Waraka Na. 5 umekuwa mgumu kutokana na kutokuwepo mwongozo mahsusi wa namna ya kuutekeleza. Hivyo basi, ili kuwa na utekelezaji moja, Serikali imeona ni vema kutoa Mwongozo wa Utekelezaji wa Waraka Na. 5 kwa Wizara, Idara, Sekretarieti za mikoa,Wakala za Serikali na Mamlaka ya Serikali za Mitaa. Hivyo, Mwongozo huu unaelekeza namna ya kutekeleza vipengele vilivyoainishwa ndani ya waraka husika na hivyo kuwa na matumizi sahihi ya TEHAMA ndani ya Serikali. Mwongozo huu unahimiza waajiri na watumishi wa umma kufuata maelekezo na utaratibu bora katika matumizi mbalimbali ya TEHAMA na vifaa vinavyohusiana na teknolojia hiyo ikiwemo matumizi ya barua pepe, vitunza kumbukumbu na huduma za mtandao. Aidha, mwongozo unatoa maelekezo na taratibu zinazotakiwa kufuatwa pale inapotokea vifaa vya TEHAMA vinahitaji kufanyiwa matengenezo ama kuondolewa katika matumizi.

SOMA NA HII:  Akaunti ya Twitter ya mwanzilishi wa McAfee VirusScan yadukuliwa

Ni matumaini ya Serikali kuwa mwogozo huu utatumiwa kwa ukamilifu na Taasisi zote za Umma ili kuleta mafanikio chanya yaliyokusudiwa na wakati huo huo kuhakikisha kuwa siri za Serikali hazivuji kwa kutumia mwanya wa TEHAMA. Mwisho, kama teknolojia hii ikitumika kwa usahihi itasaidia Serikali kupunguza gharama za uendeshaji na kuongeza ufanisi na pia kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi na wadau wengine.

Celina O. Kombani
Waziri wa Nchi
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma


Bonyeza hapa kusoma Mwongozo wa matumizi bora, sahihi na salama ya vifaa na mifumo ya TEHAMA serikalini.

Mada zinazohusiana

Zinazohusiana

TOA MAONI

Kumbuka Ni Muhimu Kuandika Jina Lako