Sambaza:

NAKUMBUKA miaka kadhaa iliyopita sanaa haikuwa sehemu ya biashara, hakukuwa na msanii aliyefanya kazi akitegemea kupata kipato cha kuendesha maisha yake.

Wasanii wengi walitegemea ajira nje ya sanaa. Ziwe za kujiajiri au kuajiriwa na sanaa ilikuwa ni sehemu tu ya kujifurahisha nakuusogeza muda uende wakati ule wa jioni au mapumziko. Huko ndipo ilipotoka sanaa hii tunayoiona hivi sasa.

Miaka imekwenda mbio sana na utandawazi umechagiza mabadiliko kwenye tasnia ya burudani hasa muziki na filamu. Hivi sasa sanaa ni biashara, watu wanauza na kununua kazi za sanaa, wasanii hata Serikali mbalimbali duniani hujiingizia mapato kutokana na kazi za wasanii.

Utandawazi umeleta wigo mpana wa biashara kwenye sanaa hasa muziki na kufanya vyama mbalimbali kuundwa kwa lengo la kutetea masilahi ya wasanii na sanaa yao kwa ujumla.

Kwa ufinyu wa nafasi na muda, leo napenda tuutazame muziki wa kizazi kipya nchini ambao kwa hatua uliyofikia msanii mkubwa na mdogo anaweza kuuza ngoma zake licha ya kipato kutofautiana kutokana na ukubwa wa majina yao.

Wasanii huuza nyimbo zao kwenye maduka ya mtandao na kujiingizia kipato pia wamekuwa wakipata dili za matangazo ya kibiashara hivyo kukuza wigo wa kipato chao kupitia kazi ya sanaa wanayoifanya.

Kutokana na ushindani unavyozidi kukua kadiri ya siku zinavyokwenda ndiyo hivyo hivyo ubunifu katika biashara ya muziki unaongezeka. Msanii hulazimika kufuata soko linataka nini kwa wakati huo na siyo kufanya tu sanaa kwa kujitolea kama ilivyokuwa zamani. Hii ni kazi na ujira ni lazima.

SOMA NA HII:  Vidokezo 8 rahisi jinsi ya kukuza tukio lako kwenye LinkedIn

Sasa hapo kwenye kuongeza thamani ya bidhaa ya sanaa ndiyo kuna shida katika uelewa wa baadhi ya wasanii juu ya kutambua masoko yao halisi ya muziki. Kabla hujafanya biashara ni lazima ujue bidhaa yako utaiuza kwenye soko lenye watu wa aina gani.

Hivyo hivyo kwenye muziki, unapotaka kufanya muziki au sanaa yoyote ile ni lazima utambue mashabiki wanahitaji nini hiyo itakusaidia kuuza bidhaa yako kwa wingi na utaongeza mapato yako. Kama nilivyosema hapo awali kwamba wasanii wengi wameshindwa kubaini aina ya wateja wa muziki wao, ndiyo maana tunakuta wasanii wengi wanafanya muziki unaofanana kwa sababu wasanii wengi hawajafanya upembuzi yakinifu kubaini muziki wake ni maalumu kwa ajili ya kina nani.

Aina ya muziki imekuwa ni kigezo moja wapo cha msanii wa muziki kuuza bidhaa yake, wale ambao huimba inasemekana wanauza zaidi kuliko wale wanaofanya muziki wa rap kitu ambacho siyo sahihi.

Hapo kikubwa ambacho kinaangaliwa ni soko mfano, Diamond Platnumz, ameshajitengenezea aina ya muziki wake kwa ajili ya mashabiki wake hivyo wewe unapofanya muziki unaofanana na Diamond unakuwa hauwauzii mashabiki wako bali unakuwa unafanya biashara ukitegemea mashabiki wa Diamond Platnumz. Ni lazima msanii kujitafutia, jielewe wewe ni nani kwenye muziki na unahitaji soko la muziki wako liwe na watu wa aina gani.

SOMA NA HII:  Kuweka Mkeka "Kubeti" Njia ya Kutengeneza Pesa yenye Ugonjwa

Kuna wasanii wa muziki wa rap, wanafanya vyema kwenye masoko ya muziki kuliko hata wale wanaoimba.

Hiyo imetokana na wasanii hao wa rap kutambua waongeze nini kwenye muziki wao ili waweze kufanya vizuri sokoni ndiyo maana bidhaa yao inauzika kuliko wale wanaoimba.

Siyo dhambi kubadili aina ya muziki unaoufanya kama unakuweka mbali na biashara kwenye sanaa. Navutiwa mno ninapoona wasanii wanabadili aina ya muziki wao na wanafanikiwa zaidi, huko ndiko kujitafuta kwenyewe.

Huu ndio msingi wa hoja yangu , ukiwa kama msanii jaribu kutambua soko halisi la bidhaa yako ukifanya hivyo mafanikio ni lazima.


Sambaza:

Written by Mediahuru

Tunaandika kuhusu sayansi na teknolojia kwa kutumia lugha ya Kiswahili.

Leave a Comment

Kumbuka Ni Muhimu Kuandika Jina Lako