Mbwa Kudhibiti Usafirishaji Dawa za Kulevya Uwanja wa Ndege Tanzania


Katika kudhibiti vitendo vya uhalifu, kampuni ya Maendeleo ya Viwanja vya Ndege (Kadco) kwa kushirikiana na Kikosi cha Mbwa na Farasi cha Polisi, imeanza kukagua kwa kutumia mbwa mizigo inayopitishwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia).

Akizungumza wakati wa kupokea mbwa watatu watakaotumika kudhibiti usafirishaji dawa za kulevya jana, mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira alisema Serikali imedhamiria kwa dhati kudhibiti uhalifu kwa nguvu zote.

Mghwira alisema ni muda mfupi tangu kufungwa mashine maalumu za ukaguzi zenye uwezo mkubwa kwenye uwanja huo, hatua ya kuongezwa mbwa kunaonyesha dhamira ya Serikali katika mapambano dhidi ya uhalifu.

Naye kaimu mkurugenzi mtendaji wa Kadco, Christopher Mukoma alisema vitendo vya usafirishaji dawa za kulevya kupitia uwanja huo vimedhibitiwa kwa kiwango kikubwa na ujio wa mbwa hao.

Mukoma alisema ushirikiano wa Kadco na polisi umefanikisha kuwapata mbwa hao wenye uwezo mkubwa wa kutambua vitu ambavyo vimepigwa marufuku.

Mkuu wa Kikosi cha Mbwa na Farasi cha Polisi nchini, Eugene Emmanuel alisema katika miezi michache ijayo wataongeza mbwa wengine wawili ili kufikia watano na kwamba, lengo lao ni kuhakikisha viwanja vingine vya ndege vinakuwa na mbwa wenye uwezo wa kutambua mizigo isiyo salama.

0 Comments

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ZINAZOHUSIANA