TCRA yafafanua matumizi ya alama za vidole kwenye usajili wa laini za simu


Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imesema kampuni za simu za mikononi zinaruhusiwa kusajili upya laini kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya kielektroniki inayohusisha uchukuaji wa alama za vidole.

Kaimu meneja mawasiliano kwa umma wa mamlaka hiyo, Semu Mwakyanjala alisema walishafanya majaribio kuhusu mfumo huo na kuona unafaa.

Mwakyanjala alitoa ufafanuzi huo baada ya mwandishi wa Mwananchi kuuliza kuhusu ujumbe unaotumwa kwa wateja kutoka kampuni za simu za mkononi ukiwajulisha kuhusu usajili wa laini kwa kutumia alama za vidole.

“Ndugu mteja katika kuboresha usajili wa laini za simu alama za vidole zitatumika kuanzia Februari 5, 2018. Kwa mawasiliano zaidi tembelea maduka yetu,” ni ujumbe ambao umekuwa ukitumwa kwa wateja wa kampuni za simu.

Mwakyanjala alisema mfumo huo unaotumia alama za vidole na picha ni wenye uhakika ambao ni vigumu kughushi.

“Huu ni usajili wa kielektroniki ambao unaiwezesha kampuni na mamlaka kupata taarifa mbalimbali za mteja kwa muda mfupi,” alisema.

Alisema TCRA imeziruhusu kampuni zote za simu za mkononi kutumia mfumo huo.

Akizungumzia mfumo huo, meneja uhusiano wa Airtel Tanzania, Jackson Mmbando alisema kampuni hiyo itaanza kusajili kwa majaribio.

“Ni kweli tutaanza kusajili laini kwa kutumia alama za vidole kwa sababu hiyo ndiyo njia salama ya usajili,” alisema.

Alisema katika mpango huo wa majaribio wataanza kusajili katika mikoa minne ya Dar es Salaam, Pwani, Iringa na Singida. Pia, utafanyika Zanzibar. “Katika mikoa hiyo tutaanza kusajili wateja wapya kwa kutumia alama za vidole,” alisema.

Alisema baadaye wataendelea kwa wateja wengine hata ambao walishasajili laini kupitia mfumo wa zamani. “Lengo ni kuboresha zaidi mfumo huu.”

0 Comments

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ZINAZOHUSIANA