Nyingine

Maisha … ..na michezo tuliyocheza


Ninaandika kipande hiki nikiwa sina mwelekeo wa moja kwa moja ila nimezama ndani ya fikra zangu kama mwandishi , Lakini najua ni kitu gani nataka kusema  na natumaini nitafanikiwa kufikisha mawazo yangu kwako.

Siku kadhaa zilizopita , nimekuwa na mazungumzo mazuri na rafiki yangu wa karibu sana na kwa namna fulani tukajikuta tunazungumza juu ya kukua, wazazi na  mambo yote tuliyopitia utotoni.

Katika kukua kwetu tumepitia “kupanda na kushuka” pia heka heka zisizokwisha “Kupanda” kunawakilisha nyakati nzuri na “kushuka” kunawakilisha nyakati ambazo mambo hayakuwa mazuri  lakini kitu muhimu zaidi  ni kuwa kukua kwetu kulikuwa na furaha sana.

Kama mtoto, maisha hayakuwa magumu sana na kulikuwa na vitu vichache vya kuhofia au hakuna kabisa. Tuliamka Jumamosi tukiwa na mawazo ya “michezo ya mitaani” katika akili zetu hata kama si michezo yote ya mitaani ilikubaliwa na wazazi wetu.

Tuliendesha “magurudumu ya baiskeli ” na “matairi ya gari” kutoka mtaa moja hadi nyingine (Kutoka barabara ya Shule ya msingi Azimio-Kitisi-mpaka Mji Mwema na kurudi tena barabara ya Azimio-Makambako).

Ndio michezo hii ilikuwa na viwango( Nacheka). Kusukuma “matairi ya gari” kwanza , ulikuwa unaendesha “sahani” baada ya hapo unahamia kwenye “magurudumu ya baiskeli” kabla ya kuhamia ngazi ya mwisho “matairi ya gari” .  Wakati hanger ya chumu ya kuwekea nguo ilitumika “kuendesha” gurudumu au sahani, fimbo ilitumika “kuendesha” matairi ila yote hayo yalihitaji uwe na aina fulani ya ujuzi. Muda mwingine tuliandaa
‘mashindano ya mtaa” na washindi walionekana kama miungu watu. Baadhi yetu tuliyapa majina “magurudumu” na “matairi” na yalikuwa na sehemu maalumu ya maegesho.

SOMA NA HII:  Idara ya Habari (MAELEZO) Yapokea Msaada wa Vifaa Kutoka Ubalozi wa China

Kama unafikiri “kusukuma magurudumu” ilikuwa raha zaidi ,mimi nakwambia kucheza mpira wa vindude ndo kulikuwa mpango mzima.

Kama ilivyo kwa soka la kawaida, unaweka timu yako ya wachezaji 11 na wengine wa akiba pembeni . Tulicheza kwa kutupia “fimbo” au kidole gumba na kidole kwanza kwa pamoja.

Baada ya muda tukaacha kucheza mpira wa vindude na kuhamia kwenye mpira wa uwanjani na tulishindana na mitaa ya jirani .Tulichangia (Sh50, sh100, sh200) kwajili ya kununua vitu mbalimbali kama pipi na glucose.  Wote tulicheza kushinda kombe ambapo mala nyingi vilikuwa ni vitu vitamu vya kula.

Maisha yalikuwa kama play station ukizingatia kulikuwa na muda wa kwenda kula nyumbani. Sikujua ada yangu ya shule inalipwa vipi, na wala hilo halikunisumbua. Nilikua naangalia vitu vizuri tu kwenye maisha.

Sijui kama michezo hii bado inachezwa na watoto wa siku hizi ila nakwambia hii ndo ilikuwa njia nzuri ya kuwa na busara mtaani kwa wakati huo kuliko kucheza mchezo wenyewe.

Samahani kama haujapitia mchezo wowote enzi za utoto wako….pengine umekulia kwenye PS na Xbox .

Ndio tunapoongelea matukio na kumbukumbu za utotoni , jambo moja lipo wazi kabisa , kumbukumbu za utotoni zinatofautiana kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine.

Tafadhali acha ushahidi wako kama kumbukumbu zako zinaendana na zangu pia tuambie unakumbuka mchezo gani wa enzi za utoto wako.

SOMA NA HII:  Hali ni mbaya sana kwa tovuti za Pirates na wazee wa Torrent

Zinazohusiana

TOA MAONI

Kumbuka Ni Muhimu Kuandika Jina Lako