Kuweka Mkeka “Kubeti” Njia ya Kutengeneza Pesa yenye Ugonjwa


Kwa Mtanzania wa sasa ukisema neno “kubeti” anakuelewa moja kwa moja unachomaanisha, labda kwakuwa yeye mwenyewe ameshacheza au watu anaowajua, pengine hata kuwaona tu wengine.

Hii ni michezo ya bahati nasibu ambapo kampuni mbalimbali duniani huweka viwango fulani kwa mashabiki wa michezo hiyo kutabiri mwenendo wa mchezo husika utakavyokuwa au utakavyoisha.

Hapa Tanzania mchezo maarufu zaidi ni soka. Hivyo mashabiki wa mchezo huo hutabiri mambo kadhaa katika mchezo husika ikiwemo wafungaji wa magoli, idadi ya magoli kwenye mechi husika, magoli yatafungwa kipindi kipi cha mchezo, mechi ikiisha matokeo yatakuwaje, n.k.

Watu wakifatilia “mikeka” ya michezo ya siku ili wabeti

Gharama ya kubeti inaanza kwa bei ndogo sana ya shilingi 500 ambapo unanunua tiketi ambayo itakuwa na mechi unazotabiri. Kwakuwa shilingi 500 inaonekana ni ndogo sana watu wengi wenye kipato kidogo kama wanafunzi wa shule za sekondari na waendesha bodaboda, inakuwa rahisi kushiriki. Baada ya kushinda na  kushindwa mara kadhaa, ni kawaida sana kuona vijana hawa wakishindwa kabisa kuizungumzia michezo bila kuihusisha na kubeti.

Mazoea haya ya kutengeneza pesa kwa njia za mkato yanatengeneza ugonjwa, ugonjwa ambao kimsingi unakusababisha kutokuwa makini na shughuli itayokutengenezea maisha yako na kuzingatia sana njia za mkato za kubeti.

Halitakuwa jambo la kushangaza kabisa miaka kumi ijayo kuona watu hawa wakitegemea kuendesha maisha yao kwa kucheza kamari muda mwingi kwenye makasino kwa maana msingi wa wao kuipenda michezo ya aina hii wanakuwa wameshautengeneza kwa miaka zaidi ya kumi.

Kwa makusudi kabisa, wazazi wana jukumu kubwa kuhakikisha wanawapa muongozo watoto wao ili waelewe madhara ya kuzoea kupita kiasi michezo ya aina hii na wajue athari zake kimaisha. Bila hivyo tutakuja kutengeneza kundi la vijana lililoathirika kwa kucheza kamari.

0 Comments

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ZINAZOHUSIANA