Sambaza:

KAMPUNI ya Simu Tanzania (TTCL) imefanya mabadiliko makubwa ya nembo yake pamoja na kuzindua huduma ya mtandao wa kisasa wa 4G LTE ikiwa ni muendelezo wa mpango wa kufanya mabadiliko ya kibiashara kwa kampuni hiyo.

Nembo hiyo mpya ya TTCL na huduma ya 4G LTE vimezinduliwa leo jijini Dar es Salaam na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa huku akiipongeza kwa hatua hiyo ya kuleta mabadiliko ya kiutendaji na uwajibikaji unaolenga kuonesha tija na ubora.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (kulia) akizinduwa nembo mpya ya Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) pamoja na kuzinduwa huduma ya mtandao wa kisasa wa 4G LTE leo jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Bodi ya TTCL, Bi. Edwina Lupembe akishiriki zoezi hilo.

Waziri Mbarawa alisema uzinduzi huo ni utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Pombe Magufuli la kufanya kazi kwa bidii, maarifa, uadilifu na kufikia viwango vya juu kabisa vya kutoa huduma kwa umma sambamba na mpango mkakati wa TTCL kibiashara kwa kipindi cha mwaka 2016-2018.

SOMA NA HII:  #MHKutokaMaktaba!! Tujikumbushe Watangazaji wa Zamani wa Redio na TV

“Pamoja na pongezi hizi za dhati, naomba mtambue kuwa uzinduzi huu hautakuwa na maana yoyote pasipo mabadiliko ya kiutendaji utoaji huduma kwa wateja. Watumiaji wa huduma zenu wanahitaji mabadiliko ya dhati ya viwango vya huduma na utendaji ili kuwajengea imani juu ya uwezo wenu wa kuwahudumia,” alisema Waziri Mbarawa.

Kwa upande wake Ofisa Mtendaji Mkuu wa TTCL, Dk Kamugisha Kazaura alisema uzinduzi wa nembo mpya ya TTCL unaleta muonekano mpya wa kampuni unaoenda sambamba na mageuzi ambayo yanaendelea katika kuboresha miundombinu ya mtandao wa simu na data.
Alisema katika safari ya mageuzi TTCL imefanikiwa kuboresha miundombinu ya simu za mezani na mkononi kwa kuleta teknolojia ya 2G GSM, 3G, UMTS na LTE sokoni ili kwenda sambamba na ushindani wa soko la mawasiliano.
“…Teknolojia hizi zitaisaidia kuongeza ufanisi, ubunifu katika kutoa huduma ya simu za mezani, simu za mkononi na huduma ya intaneti zenye ubora wa hali ya juu na ya uhakika na gharama nafuu,” alisema Dk. Kazaura.
Alisema kwa sasa kampuni hiyo inaendelea na juhudi za kuboresha miundombinu ya mawasiliano ya data nchi nzima, hali ambayo itaongeza ubora wa huduma zetu kwa wateja wetu wote ndani na nje ya nchi.

SOMA NA HII:  Airtel ni mali ya TTCL Palifanyika Mchezo wa Hovyo - Rais John Magufuli

Sambaza:

Written by Mediahuru

Tunaandika kuhusu sayansi na teknolojia kwa kutumia lugha ya Kiswahili.

Leave a Comment

Kumbuka Ni Muhimu Kuandika Jina Lako