Mawasiliano

Jinsi ya kuhama mtandao wa simu bila ya kubadili laini

on

TANZANIA kama ilivyo nchi zingine duniani, imeshuhudia ukuaji wa sekta ya mawasiliano ambayo imechangia katika kuboresha maisha ya wananchi kijamii na kiuchumi sambamba na pato la taifa.

Ukuaji wa sekta hii umechangiwa na kuwepo kwa sera, sheria kanuni na mfumo mzuri wa utoaji leseni za huduma za mawasiliano.

Takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) zinaonesha kwamba kuanzia mwaka 2005, kulikuwa na jumla ya laini za simu za kiganjani 2,963,737 idadi ambayo imeongezeka hadi kufikia laini 40,173,783 Desemba 2016.

“Ongezeko hili la utumiaji wa huduma za mawasiliano ni lazima liende sambamba na utoaji wa huduma bora kwa wateja ili mteja apate huduma bora kwa bei nafuu,” anasema Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, James Kilaba.

Kutokana na umuhimu wa tekinolojia ya habari na mawasiliano (Tehama) katika maendeleo ya taifa, mijini na vijiji TCRA imezindua mpango maalumu wa kuhama mtandao mmoja wa simu kwenda mtandao mwingine bila kubadili namba ya simu na kueleza njia za kufuata ili kupata huduma hiyo.

Huduma hiyo ambayo jana imezinduliwa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, inampa fursa mteja kuhama kutoka mtandao mmoja wa simu kwenda mwingine bila kubadili namba na uhamaji huo unatakiwa kuwa wa hiari na si kulazimishwa au kuzuiliwa kuhama.

Kilaba anasema huduma hiyo inaanzishwa kwa mujibu wa kanuni za mwaka 2011 za Sheria ya Mawasiliano ambapo anayetaka kuhama ataondolewa usumbufu wa kuwataarifu watu wake na unampa uhuru mtumiaji kuchagua mtoa huduma anayemtaka.

SOMA NA HII:  China Kujenga Kiwanda Kikubwa Cha Kutengeneza Vifaa Vya Mawasiliano Tanzania

“Huu ni utaratibu wa hiari kwa sababu hii ni fursa ya mawasiliano kama fursa zingine ambazo zimeanzishwa za kutuma na kupokea fedha, hivyo wananchi hawatakiwi kulazimishwa kuhama au kuzuiliwa kuhama,” anasema.

Kilaba anasema huduma hiyo pia itaongeza ushindani kwenye sekta ya mawasiliano na hivyo kuwa kichocheo cha utoaji huduma bora. “Mfumo huu utatumiwa na wateja wote wanaolipia huduma kwanza na wale wanaolipia huduma baada ya matumizi.

Anapozungumzia hatua za kufuata wakati wa kuhama, Mhandisi wa Mawasiliano wa TCRA, Mwesigwa Felician, anasema hatua ya kwanza mteja anatakiwa kwenda kwenye kituo cha mauzo au kwa wakala anayetambuliwa na kueleza dhumuni lake la kutaka kuhama.

Anasema hatua hiyo, inafutiwa na mteja kujaza fomu maalumu ya maombi ya kuhamia mtandao anaotaka kuhamia. “Fomu ya maombi ya kuhama ni tamko rasmi la mteja la kukubali kutowajibika kwa madeni yoyote ambayo yanatokana na huduma ulizokuwa unapata kwa mtoa huduma wako wa awali kama yatakuwawepo.” Felician anaongeza: “Mteja atatakiwa kutoa kitambulisho chenye picha ya mhusika ambacho kinatambuliwa, mfano kitambulisho cha taifa, kadi ya mpiga kura, leseni ya udereva, pasipoti au kitambulisho chochote rasmi kinachotambulika. “Wakati wa kuhama mtandao, mteja anatakiwa kuwa na simu ya kiganjani inayofanya kazi. Hii ina maana ili kuingia kwenye mfumo huu, simu ya mtumiaji lazima iwe inatumika yaani haijafungiwa au kusimamishwa kwa muda,” anasema.

Anasema pia mteja hawezi kuhama kama ana mkopo na kama namba inahusishwa na uhalifu. Anasema mtumiaji anayetaka kuhama, ni lazima ahakikishe anahamisha fedha zilizopo kwenye akaunti ya simu au salio na muda wa maongezi anaumaliza kwanza kwani fedha hizo zitapotea akishahama.

SOMA NA HII:  Vodacom yarudisha mtaji, Hisa zarejea bei ya awali

“Kama unaona kwenye akaunti ya simu kama tigopesa, M-pesa, airtel-money kuna fedha unatakiwa ziondolewe maana katika kipindi fulani cha kuhama huduma ya kutuma na kutoa fedha haitakuwepo. “Pia kama simu yako ina salio, yaani muda wa maongezi unatakiwa uhakikishe umemalizika kwani ukihama, hutohama na muda wa maongezi, hii ni kama ‘unaposwapu’ simu,” anasema.

Felician anasema hatua ya nyingine ya kukamilisha uhamaji ni kwa mteja kutakiwa kutuma ujumbe mfupi wa maneno wenye neno ‘HAMA’ kwenda namba 15080 ambayo ni namba maalumu ya kuhama.

“Baada ya kutuma neno ‘HAMA’, mteja atapokea ujumbe mfupi wa maneno utakaomjulisha kuwa ombi lake limekubaliwa. “Endapo namba yako haikuzuiliwa au kusimamishwa kwa muda kutokana na kutokamilisha malipo ya madeni ya mtoa huduma wako wa awali, maombi yako yatashughulikiwa na utajulishwa kwa ujumbe mfupi wa maneno maendeleo ya mchakato huo,” anasema Felician.

Anaongeza: “Mteja anatakiwa yeye mwenyewe kutuma neno HAMA ili kuonesha uhiari wake wa kuhama, na akishajibiwa kukubaliwa mtoa huduma mpya atampatia laini ya mtandano aliohamia. Anasema baada ya kuhama mteja ataweza kupata huduma za kupiga na kupokea simu na ujumbe mfupi wa maneno zitaendelea kama kawaida.

“Mchakato wa kuhama kutoka mtandao mmoja kwenda miwingine unatakiwa kufanyika ndani ya saa kadhaa kama mhusika namba yake haitakuwa na vikwazo vya kumfanya ahame na haitazidi siku mbili pekee.

“Wakati namba yako ya zamani ikiwa imehamishiwa kwa mtoa huduma mpya, laini yako ya awali haitatumika tena ingawa watu wanaokupigia simu watakupigia kwa namba ile ile na utaendelea na huduma kama kawaida,” anasema Felician.

Felician anasema mteja anaweza kuhama mitandao atakavyo, lakini mchakato huo anatakiwa kuufanya baada ya kupitia siku 30 tangu ulipohama mtandano wa kwanza.

“Ukitoka kwa mtoa huduma A na ukaamua kuhamia kwa mtoa huduma B, ukitaka kwenda kwa mtoa huduma mwingine au kurudi kwa yule wa awali unatakiwa kuwa ndani ya mtoa huma huyo mpya kwa siku 30. “Kama mteja ndio kwanza ameanza kupata huduma ya mtoa huduma (mteja mpya kwa mtoa huduma) basi atatakiwa kuendelea kupata huduma zake kwa mtoa huduma huyo mpaka baada ya siku 60 ndio ataruhusiwa kuhama.”

Huduma hii katika Afrika imeanzishwa katika nchi za Misri, Kenya, Sudan, Afrika Kusini, Ghana, Nigeria, Senegal na Morocco na nchi za Rwanda na Namibia zipo katika mchakato wa kuanzisha.

About Mediahuru Team

Hapa Mediahuru, tunaandika kuhusu sayansi na teknolojia kwa kutumia lugha ya Kiswahili. Tumejikita kuhakikisha hupitwi na habari yoyote ya teknolojia, endelea kuwa nasi kila siku. - MediahuruDotCom | info@mediahuru.com

Recommended for you

Leave a Reply

Your email address will not be published.