Simu za Mkononi

Password inavyoweza kuokoa au kuangamiza maisha ya mtu

Zipo simulizi kadhaa za baadhi ya watu waliofanikiwa kuokoa uhai wao na wapendwa wao kwa kutoweka nywila ‘password’ kwenye simu zao za mkononi.

Hata hivyo, baadhi hupendelea kuweka neno hilo la kufungulia simu kutokana na sababu mbalimbali, kubwa ikiwa usalama wa simu zao.

Nywila inasaidia kufanya taarifa muhimu na za siri zilizomo kwenye simu zisiweze kufikiwa na mtu asiyeimiliki hadi kwa mtu anayeijua na hivyo huzuia watu wengine kutumia simu yako pindi inapoibiwa.

Baadhi ya watumiaji wa simu hizo na wachambuzi mbalimbali wanasema kuna uzuri na ubaya wa kuweka nywila kwenye simu.

Mmoja wa watumiaji wa simu, Nancy Nyalusi amesema tangu mdogo wake Hitra Nyalusi alipopata ajali mbaya ya barabarani na simu yake isiyo na nywila kutumika kwa ajili ya mawasiliano, hajawahi tena kuweka.

“Mdogo wangu aliwahi kupata ajali ya pikipiki maeneo ya Kimara, alijibamiza kichwa na akapoteza fahamu, bahati nzuri askari wa usalama barabarani alikuwa karibu, akakimbilia simu yake kisha akatafuta jina lililoandikwa mama, na kupiga,” amesema.

Alisema taarifa hiyo iliwafanya wawahi eneo la tukio kisha kumuwahisha hospitali kwa ajili ya matibabu.

Hitra alisema huwa hapendelei kuweka nywila kwenye simu yake hasa eneo la kupiga japo wakati akifanya hiyo, hakujua kama ipo siku itatumika kuokoa maisha yake.

Mkazi mwingine wa Magomeni jijini Dar es Salam, Athman Juma, alisema mke wake alipoteza maisha baada ya mtoto wake kushindwa kupiga simu yenye nywila kuomba msaada wakati mama yake alipozidiwa kwa shinikizo la juu la damu.

SOMA NA HII:  Simu ya Infinix Smart X5010 – “Be Smart , Be You”

“Mtoto wangu wa darasa la tatu alishindwa kupiga simu ya kuomba msaada kwa sababu mke wangu aliweka ‘password’, na kibaya zaidi, geti lilikuwa limefungwa hivyo hata alipopiga kelele, nje hawakusikia,” amesema.

Hata hivyo, alisema watu walipofika, mke wake alikuwa ameshafariki kutokana na kukosa msaada wa haraka.

Calvin Joseph, mkazi wa Kibaha alisema simu yake ameweka nywila kwa ajili ya usalama wa vitu vilivyomo ndani.

“Kuna wakati mke wangu huwa anachukua simu na kupekua. Simu isipokuwa na nywila huwa tunagombana sana ndio maana niliamua kuiweka. Sasa hivi akichukua mpaka aniulize nimfungulie. Nywila inasaidia,” alisema.

Mtaalamu wa saikolojia, Frank John alisema wanaopendelea kuweka nywila wanaepuka migogoro ya mahusiano yao.

Mtaalamu wa Mitandao, Dk Barack Mwambeta amesema: “Kuweka password kwenye simu sio muhimu kabisa hasa kwa mtu mwaminifu. Simu hubeba vitu vingi muhimu vyenye uhusiano wa karibu wa muhusika mfano ukipata ajali na ukashindwa kujitambua, msaada wako wa kwanza wa kuwapata ndugu zako ni simu.

Zinazohusiana

TOA MAONI

Kumbuka Ni Muhimu Kuandika Jina Lako