Nyingine

Fanya haya katika ujana wako kama Unataka kujitegemea kifedha mapema

Vijana wengi wana ndoto za kujitegemea kimaisha haraka iwezekanavyo. Watalaamu wa mambo ya fedha, mitaji na tafiti za kiwekezaji wanasema ni asilimia 10 tu ya watu duniani hufanikiwa kufikia hatua ya kujitosheleza katika maisha kimahitaji, lakini pia ni asilimia 1 tu ya watu hufanikiwa kuwa mabilionea na ubilionea unaozungumziwa hapa ni ule wa mabilioni ya dola za Kimarekani, sio shilingi zetu za Kitanzania. (Dola 1 ni sawa na shilingi 2,200 za Kitanzania). Haya ni mambo 11 ambayo wataalam wanasema kijana anapaswa kuyafanya walau kabla hajafikisha miaka 35 ili kuwa na uhakika wa mafanikio kiuchumi miaka yake ya uzeeni (kuanzia miaka 40 na kuendelea).

Mambo hayo 11 ni haya hapa:

1. Tia bidii katika kutafuta. Usiote fedha, tafuta fedha. Usiishie kuota mafanikio, yatafute. Kama unaota kuwa mkulima kubwa, panga mipango kuelekea kutimiza lengo hilo. Usiote tu kwamba siku moja nitakuwa mkulima mkubwa, ndoto bila mipango zinabaki kuwa ndoto.

2. Wekeza katika mambo mbalimbali. Mfano kama una uwezo wa kumiliki bodaboda, kwa nini usiwekeze katika jiko ambalo utatumia bodaboda hiyo hiyo kufikisha chakula wateja wanapotoa oda zao? Kama unawekeza katika mgahawa kwa nini usiwekeze pia katika ukulima iwe moja kwa moja au kuingia ubia na wenye wazo kama lako? Ukiweka mayai yote kwenye kapu moja hasa ujanani katika ulimwengu wa biashara na uchumi, unajiandalia anguko.

3. Weka akiba ili uitumie kuwekeza, usiweke akiba kama kipofu ili tu uone una hela kwenye akaunti. Hela kwenye akaunti unaweza kutunza kama tahadhari lakini si akiba yote. Tumia sehemu ya akiba kuwekeza kupata faida.

4. Usichukue muda mrefu sana bila sababu kufanya maamuzi. Dunia inakwenda kwa kasi, unachokiwaza mwaka huu ukifanye ukashindwa kukifanya usidhani mwakani mazingira ya kukifanya yatakuwa yale yale kama ya mwaka huu.

5. Usifanye show-off zisizo na msingi. Kama unaingiza milioni 20 kwa mwezi katika biashara zako na unatumia gari la milioni 9 na uko sawa huna tatizo unaweza kuendelea kulitumia. Kikubwa si aina gani ya gari unaendesha bali kiasi gani mawazo yako ya kukua kiuchumi yanafanikiwa.

6. Badilisha mtazamo wako kuhusu mafanikio. Amini kwamba mafanikio yanawezekana kama una fikiri vizuri (thinking) na unaweka mawazo yako katika utendaji. Amini kwamba mafanikio ni kitu ambacho kila binadamu anaweza kupata kama akijipanga vizuri. Mafanikio hayajaandikiwa watu fulani peke yake.

7. Wekeza ndani yako. Jielimishe kuhusu biashara, uwekezaji, namna ya kufanya maamuzi yenye tija na kadhalika. Unaweza kufanya hivi kwa kusoma vitabu, kuzungumza na waliokutangulia na kufanikiwa, kuhudhuria mikutano yenye malengo kama hayo, na kuendelea.

8. Tambua thamani yako na isimamie. Mfano kama wewe unajua thamani yako ni shilingi 100 kamwe usikubali iwe shilingi 10. Hakuna aliyewahi kufanikiwa na kufikia level yake kamili bila kujua thamani yake ni kiasi gani.

9. Weka malengo. Usiishi kama kipofu kila siku ukiamka unasubiri uone siku inaendaje. Amua wewe siku yako unataka iende vipi sio uiache siku ikuamulie.

10. Kaa na watu ambao watakujenga. Marafiki, mwenza, familia, na kuendelea. Watu unaotumia muda wako mwingi ukiwa nao wana athari kubwa sana (chanya au hasi) katika maisha yako.

11. Mtangulize Muumba wako mbele katika mambo yako kadiri imani yako inavyokuelekeza.

Credit: Sifaeli Ruwa’aichi

Soma na hizi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Close