Mawasiliano ya simuTanzania

Dodoma hakutakuwa na tatizo la mawasiliano

Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) imeziondoa hofu taasisi za umma zinazohamia mjini Dodoma kuhusiana na upatikanaji wa mawasiliano.

TTCL imesema itaendelea kuzihudumia taasisi hizo bila shida ili ziendelee kutekeleza majukumu yao kikamilifu kwa wananchi.

Kauli hiyo ilitolewa juzi jijini Dar es Salaam na Meneja Mawasiliano wa kampuni hiyo, Nicodemus Mushi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Idara ya Habari ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Serikali kwa taasisi zake kuwasiliana na umma na kutoa ufafanuzi wa hoja mbali mbali.

“TTCL imejipanga kufanikisha azma hii ya Serikali ya kuhamia Dodoma. Tupo tayari na tunao uwezo mkubwa wa rasilimali watu, vifaa na utaalamu wa kutosha katika kutoa huduma za mawasiliano.

“Nitumie fursa hii kuziomba taasisi zote za umma zinazohamia Dodoma kutumia huduma za TTCL ambazo siku zote zimethibitika kuwa ni huduma bora, za uhakika na zenye gharama nafuu,” alisema Mushi.

Akizungumzia mipango ya kampuni hiyo kuboresha huduma zake, Mushi alisema kwa kutumia fursa iliyopo katika Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, TTCL inaendelea kutekeleza kwa vitendo wajibu wake kwa umma kwa kuwa mstari wa mbele katika kuziunganisha kampuni, taasisi, ofisi za Serikali, mashirika ya umma na binafsi sambamba na wateja waliopo nchi jirani ili waweze kupata mawasiliano ya uhakika wakati wote.

SOMA NA HII:  Kampuni ya Simu ya TTCL yafutiwa deni la Sh76 bilioni

Kwa sasa tunao Mpango Mkakati wa Biashara wa miaka mitatu (Strategic Business Plan 2016-2018) unaolenga kuboresha na kuleta huduma mpya katika soko, kuongeza tija na uwajibikaji ili kutoa huduma bora kwa wateja wetu hasa tukizingatia kuwa TTCL ni mhimili mkuu wa mawasiliano nchini.

Akifafanua kuhusu hatua muhimu zilizochukuliwa na TTCL hadi sasa kutekeleza mpango wa mabadiliko, alisema ni pamoja na kuboresha miundombinu ya mtandao wa simu na data, kuondoa mitambo chakavu, kuleta huduma bora na zenye kukidhi mahitaji.

Aidha alisema TTCL imeboresha miundombinu ya simu za mezani na mkononi kwa kuleta teknolojia ya GSM -2G, UMTS-3G na 4G LTE sokoni ili kwenda sambamba na ushindani wa soko la mawasiliano nchini.

“Teknolojia hii itasaidia kuongeza ufanisi katika kutoa huduma ya simu za mezani, simu za mkononi na huduma ya intaneti yenye kasi zaidi.

“TTCL inaendelea na juhudi za kuboresha miundombinu ya mawasiliano ya data nchi nzima (IP Core Network, IP transport Network, Metro Network).

Mushi alisema hiyo itaongeza ubora wa huduma zetu kwa wateja wetu kama vile wizara, idara na taasisi za umma, Serikali za mitaa, taasisi za fedha, kampuni za umma na binafsi na wadau wengine wa ndani na nje ya nchi.

Alisema kufanikiwa kwa mpango huo kutaleta mabadiliko chanya katika huduma za kijamii kama vile elimu, afya, biashara na uwekezaji, ujasiriamali, kilimo, ufugaji na huduma nyingine ambazo kwa kiasi kikubwa zinahitaji mawasiliano ya uhakika ili kufanyika kwa ufanisi,” alisema Meneja huyo wa Mawasiliano wa TTCL.

SOMA NA HII:  PROF, MBARAWA AZINDUA BODI MPYA YA TTCL, AITAKA KUJIPANGA KUINGIA KATIKA USHINDANI WA KIBIASHARA
Mada zinazohusiana

Zinazohusiana

Leave a Reply

Your email address will not be published.