Biashara Mtandaoni

BRELA: Sasa unaweza kusajili Kampuni na Biashara kwanjia ya Mtandao

on

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) unatarajia kuzindua mfumo wa usajili wa kampuni na biashara kwa njia ya mtandao.

Baada ya mchakato wa muda mrefu, mfumo huo utazinduliwa mwezi ujao lakini kila Mtanzania anapaswa kuwa na kitambulisho kinachotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) ili kuhudumiwa kwa urahisi.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Brela, Frank Kanyusi amesema wageni kutoka nje ya nchi wanatakiwa kutumia namba za pasi zao za kusafiria.

“Huduma hii imekamilika tangu Juni 2 na itazinduliwa rasmi Agosti mwaka huu. Kitambulisho cha taifa ni muhimu kwa sababu ni hitaji la kwanza kufanikisha usajili,” alisema Kanyusi.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Brela, Frank Kanyusi

Awali, huduma ya mtandao ilikuwa ni kwa ajili ya majina ya biashara lakini sasa imepanuliwa na kuruhusu usajili wa majina ya kampuni.

SOMA NA HII:  Makosa 6 ya kifedha yanayofanywa na wamiliki wa biashara mpya na jinsi ya kuyaepuka

Licha ya Nida, Brela sasa inashirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita) na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwenye huduma zake.

Baada ya mhusika kutembelea tovuti ya Brela na kuingiza namba ya kitambulisho chake cha taifa au pasi ya kusafiria, Kanyusi alisema taarifa hizo zitapelekwa TRA ambao watatoa namba za utambulisho wa mlipa kodi itakayokuwa pia na cheti cha kampuni.

“Tumeamua kufanya hivi ili kupunguza mizunguko kwa sababu zamani mtu akitaka kusajili jina la kampuni au huduma nyingine kutoka Brela alitakiwa kuzunguka ofisi nyingi kupata uhakiki wa taarifa zake, lakini sasa taarifa zote zinapatikana kwa wakati mmoja,” alisema.

SOMA NA HII:  Baada ya Kauli ya JPM, Ifahamu Sheria ya Takwimu na Madhara Yake

Licha ya mabadiliko hayo, Kanyusi ameeleza kuhusu kuhamishwa kwa huduma ya kutoa leseni Daraja A kutoka ofisi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwenda Brela.

“Kuanzia Julai 15, Brela itaanza kutoa leseni hizo. Waziri wa Viwanda ameshaidhinisha Ili wateja wapate huduma zote katika jengo moja,” alisema.

About Mediahuru Team

Hapa Mediahuru, tunaandika kuhusu sayansi na teknolojia kwa kutumia lugha ya Kiswahili. Tumejikita kuhakikisha hupitwi na habari yoyote ya teknolojia, endelea kuwa nasi kila siku. - MediahuruDotCom | info@mediahuru.com

Leave a Reply

Your email address will not be published.