Sambaza:

Siku hizi watu wanapambana na ufukara kwa mbinu nyingi. Zipo zilizo halali na zipo zilizo haramu. Ndio maana utaona matukio ya ajabu yamekuwa yakifanyika kila kukicha.

Katika kukabiliana na ukata wa maisha, kumeibuka kundi la vijana wengi wakilazimika kujiunga na miradi ya shughuli za usanii wa aina kadha wa kadha. Muziki ni sanaa moja wapo.

Ingawa bado si ajira iliyorasmishwa, muziki wa kizazi kipya umeokoa vijana wengi katika mapambanao ya kuondokana na dhiki imekuwa njia kwa vijana kubadili maisha yao, muziki huu umefanikiwa kuziteka nyoyo za wananchi wa rika zote.

Ni kwa sababu hiyo, muziki wa kizazi kipya umesaidia kueneza jumbe mbalimbali na  kuwahamasisha wananchi kuhusu masuala ya kimaisha.

Sitaki kubeza kazi nzuri za baadhi ya wasanii, ambao ukisilikiza mistari yao, utagundua kuwa hawakukimbilia muziki kujiokoa na ukosefu wa ajira. Ni watu wenye vipaji. Nyimbo zao zimebeba dhana kamili iiyobebwa katika fani inayokidhi haja.

SOMA NA HII:  Kukua Kwa Teknolojia na Kazi 7 Zinazoelekea Kutoweka

Wanatuelimisha, wapo wanaokemea tabia zisizopendeza, zinazofanywa na baadhi ya watanzania. Wengine wanasihi jamii kubadilika, kazi ambayo ni nadra kufanywa kwa dhati na wanasiasa wetu. Huo ni upande wa kwanza wenye matumaini.

Hata hivyo katika upande wa pili, nasikitika kusema kuwa Bongo flava imevamiwa na wababaishaji wasiojua wajibu wao katika jamii. Wababishaji wanaopenda sifa tu kwa kuimba nyimbo za majigambo yasiyo na msingi kwa kigezo cha kuburudisha jamii.

Ni kweli kuwa pamoja na maudhui yake, fasihi vilevile inawajibika katika kuburudisha wanajamii, ambao kimsingi hukumbana na mengi ya kukatisha tamaa na kutupunguzia ari ya kufanya kazi maana hisia zetu zinakuwa zimejeruhiwa.

Tunajua kuwa Tanzania ina matatizo mengi sana ambayo kama wasanii wangekuwa makini, wangeweza kufanya kazi  katika kuleta mabadiliko makubwa katika jamii yetu. Lakini inavyoonekana Wasanii (na kweli ni wasanii/waigizaji) wamejikita zaidi katika kupigana vijembe wao kwa wao.

Mtu anahisi kuwa fulani hampendi, basi anamtungia mistari. Huyo naye anakwazwa na mistari hiyo, anaingia studio kwa majibu. Basi alimradi ni biashara isiyo na mwenyewe. Haina kichwa wala miguu.

SOMA NA HII:  Kuweka Mkeka "Kubeti" Njia ya Kutengeneza Pesa yenye Ugonjwa

Mtu tunamjua ni masikini kama walivyo watanzania wengi, lakini unakuta katika video yake anaigiza maisha ya ufahari uliopindukia. Magari ya kifahari (ya kuazima), maisha ya ngono zembe na ulevi wa pombe uliokithiri. Mtu kama huyu bado eti anataka watanzania wajifunze kwake! Kama wapo wakujifunza kwake, basi ni wendawazimu.

Wengine wamejikita katika kutuimbia mambo ya kimapenzi zaidi, wanasahau kuwa Mtanzania mwenye njaa, hawezi kula mapenzi. Mtanzania anayetishiwa na umasikini hawezi kusaidiwa na aina ya muziki tunaousikia katika vituo vya redio na luninga.

Muziki wa Bongo Flava hauwezi kuisaidia jamii kama wasanii wenyewe wataendelea kuimba imba vitu visivyo na kichwa wala miguu. Mambo hayo tuwaachie wa- magharibi ambao walishatuibia siku nyingi, wamesahau kama kuna mtu katika dunia ya leo, anaweza kuamka asijue wapi pa kuanzia katika kuusaka mlo wa mchana! Kama hawana shida hiyo, hata ukiimba upuuzi wowote watakuelewa, maana wameshiba!

SOMA NA HII:  Mfahamu Mwanzilishi Wa Kampuni ya Simu za Tecno - Tecno Mobile

Nimewahi kumsikia msanii moja akiisifu pombe na maisha ya ngono, nikajiuliza, hivi hana cha kuimba? Anasifu pombe ili iweje, kuwafanya watanzania wajue umuhimu wa ulevi?

Nafikiri hii ndio sababu hatushuhudii wasanii wetu wakifanya vizuri kwenye mashindano ya kimataifa. Hawashindi kwa sababu nyingi. Moja ikiwa ni udhaifu wao wa kuimba mambo yasiyoshahibiana na hali halisi ya Maisha ya Waafrika.

Nawashauri wajifunze kwa wenzao (weusi kama wao) lakini wanajua nini cha kufanya unapotaka kuingia studio. Wanatafiti ni kipi kimepungua katika jamii zao, nini kinahitajika na hivyo kitungiwe wimbo.

Wapo wasanii wachache wanaojua umuhimu wa Utamaduni wa mwafrika. Wengine kama hawatakuwa tayari kubadilika, waimbe maisha halisi ya watanzania, waishauri jamii kugeuka fikra, basi tutalazimika kugeukia rekodi za nje.

Sambaza:

Written by Mediahuru

Tunaandika kuhusu sayansi na teknolojia kwa kutumia lugha ya Kiswahili.

Leave a Comment

Kumbuka Ni Muhimu Kuandika Jina Lako