Sambaza:

RIPOTI ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2015/16 iliyowasilishwa bungeni April 13, imebaini udhaifu katika mradi wa bomba la usafirishaji gesi asilia kati ya Mtwara na Dar es salaam.

Baadhi ya mambo aliyoeleza CAG, Prof. Mussa Assad, katika ripoti yake ni matumizi ya bomba hilo kuwa chini ya kiwango na wateja wa gesi asilia hulipa bei inayofanana ilihali wapo umbali tofauti.

Mengine ni kutokulipwa kwa ankara za mauzo ya gesi asilia kutoka Shirika la Umeme (Tanesco) kwenda Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC), kuwapo kwa kipengele cha mkataba wa mkopo kisichoridhisha na tofauti ya bei ya gesi kwa wauzaji wa gesi kwa Tanesco.

Pia, tatizo la mifumo ya usalama katika kituo cha kinyerezi, mikataba ya uuzaji wa gesi yenye kipengele cha serikali kulipia gesi hata kama haijatumia gesi hiyo na mgogoro usio na ufumbuzi wa bei ya mabaki yaliyotokana na uzalishaji wa gesi.

SOMA NA HII:  Je una bashiri "kubeti" ili kujikwamua na matatizo ya kimaisha ?

CAG alisema kwasasa Tanesco ndiyo mteja pekee wa gesi ambapo anatumia wastani wa futi za ujazo milioni 46.61 kwa siku ambapo makubaliano yalikuwa ni kutumia futi za ujazo milioni 80 kwa siku. Tanesco ndiyo mteja pekee aliyeunganishwa kwenye bomba hilo na anatumia asilimia sita ingawa gesi ilikusudiwa kuwa na matumizi mengi .

“Nashauri jitihada zaidi ziongezwe katika kuhakikisha wateja zaidi wa gesi asilia wanapatikana ili mkopo uweze kulipwa kabla ya marekebisho ya ulipaji ambayo yataongeza gharama kubwa kwa serikali,” alisema Prof. Assad.

Prof. Assad alisema matumizi ya bomba hilo yapo chini ya kiwango kwa asilimia 94 kwa sababu lilijengwa ili kuwezesha usafirishaji wa gesi asilia kwa ajili ya matumizi ya kuzalisha umeme, viwandani, kupikia majumbani na kwenye magari.

“Kiasi hicho ni pungufu futi za ujazo milioni 737.39 kwa siku ili kujaza bomba,” anasema CAG katika ripoti. “Hii ni tofauti na mkataba wa mauziano na Tanesco inatumia gesi kwenye mitambo sita ya uzalishaji umeme.”

Aidha, CAG alisema kutoza bei ya gesi inayolingana kwa wateja wa gesi asilia waliopo Dar es salaam na waliopo jirani na chanzo cha gesi sio njia sahihi ya kuhamasisha upatikanaji zaidi wa wateja.

SOMA NA HII:  Idara ya Habari (MAELEZO) Yapokea Msaada wa Vifaa Kutoka Ubalozi wa China

Prof. Assad alishauri TPDC kuandaa rasimu ya bei ya gesi itakayotofautisha bei za gesi zitakazokuwa zikilipwa na wateja mbalimbali kulingana na umbali kutoka chanzo cha gesi.

CAG alibainisha Tanesco haijailipa TPDC kiasi cha dola za Kimarekani milioni 61.35 za ankra ya mauzo ya gesi asilia.

Alisema TPDC na Tanesco walikubaliana serikali iweke dhamana benki kiasi kinachoweza kulipa mauzo ya gesi kwa miezi mitatu au zaidi kwa ajili ya TPDC na dhamana hiyo iwepo hadi pale Tanesco itakapolipa madeni yanayohusu mauziano ya gesi hiyo.

“Serikali haijaweza kuweka dhamana hiyo, (na) hadi Desemba 2016 jumla ya deni la mauzo kiasi cha dola za kimarekani milioni 61.35 sawa na Sh. bilioni 133.4 kilikuwa kimelimbikizwa bila kulipwa na Tanesco,” alisema.

Alisema hali ya kuchelewa kuilipa TPDC inasababisha TPDC kuchelewa kuyalipa makampuni yanayouza gesi na hivyo kuongeza hali ya sintofahamu kwenye ulipaji wa mkopo wa benki ya Exim ya China.

SOMA NA HII:  Teknolojia 5 Maarufu kwenye Magari Kwa Sasa

Benki hiyo ilitoa mkopo wa masharti nafuu dola za Kimarekani bilioni 1.225 kwa ajili ya ujenzi wa bomba hilo lililojengwa na kampuni ya maendeleo ya petroli na Teknolojia China (CPTDC) kwa gharama ya dola za kimarekani bilioni 1.283.

Sambaza:

Written by Mediahuru

Tunaandika kuhusu sayansi na teknolojia kwa kutumia lugha ya Kiswahili.

Leave a Comment

Kumbuka Ni Muhimu Kuandika Jina Lako