Biashara ya mtandao inafanyikaje? Malipo na Changamoto za usafirishaji bidhaa


Umekaa nyumbani unataka kununua bidhaa zako lakini hujisikii kwenda duka lolote la jirani au ‘supermarket’. Usiwaze, mambo siyo kama zamani tena.

Watu wengi hawajui kuwa kupitia simu yako ya mkononi, tabiti, au kompyuta yenye mtandao, unaweza kununua bidhaa zako na kuzipata kwa muda mfupi mlangoni kwako.

Kasi ya ukuaji wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) imefungua milango ya kununua bidhaa mtandaoni kwa kuyavuta maduka na kupunguza utegemezi wa kununua bidhaa kwa kuonana na muuzaji.

Kampuni kadhaa za nje na za ndani kama Kaymu, Hellofood, Kivuko, Jumuia, ShoppingTz na nyinginezo, zimeanzisha huduma hiyo ili kutumia fursa adhimu ya biashara katika jamvi la Tehama.

Biashara hii inafanyikaje?

Katika soko au duka la mtandaoni, mteja na muuzaji hawakutani ana kwa ana, bali kupitia mtandao kwa kuunganishwa kupitia tovuti au programu ya simu (‘app’) ambazo nyingi humilikiwa na kampuni za kijasiriamali.

Tovuti hizo huwa ni jamvi au meza ambazo wauzaji huweka taarifa zao za kina kama vile bei na aina ya bidhaa, idadi, kiwango, mwaka wa kutengenezwa (kwa bidhaa za kuisha muda) na uwezo wake.

Taarifa hizo huambatana na picha halisi za bidhaa ili kuzuia utata unaoweza kutokea mteja anapokuta bidhaa aliyonunua na kuletewa siyo ile iliyopo pichani. Programu ya kompyuta inayofanya kazi kama kikapu hutumika kufanikisha ununuzi kwa kumjulisha mnunuzi jumla ya bidhaa alizonunua na fedha anazodaiwa.

Katika tovuti hizo kuna kila aina ya bidhaa kuanzia nguo, vyakula, magari, vitabu, vifaa vya elektroniki, vipodozi, vidani, muziki, video na vinginevyo.

Malipo

Malipo katika biashara hiyo iliyoanzishwa miaka 35 iliyopita na mjasiriamali Mwingereza Michael Aldrich, yanaweza kufanyika moja kwa moja mtandaoni au wakati mteja anapopokea bidhaa.

Meneja Mkuu wa kampuni ya kuuza chakula mtandaoni, Sherrian Abdul anasema wateja wanaweza kulipia kupitia Tigo Pesa (kwa sasa) au kulipia wakati wanapokea chakula.

Pia, shoponlinetz kupitia tovuti yao wamebainisha kuwa wateja wanaweza kufanya malipo yao kupitia kampuni za malipo za Visa, Visa Electron, Paypal, Mastercard, Airtel Money na Tigo pesa.

Bidhaa kama muziki na video au programu za kompyuta unaweza kuzipakua haraka mara tu baada ya kuzilipia, wakati bidhaa kama nguo na nyinginezo zitakuhitaji usubirie kidogo inatokana na umbali wa duka lilipo na makazi yako.

Changamoto za usafirishaji bidhaa

Pamoja na mfumo wa kielektroniki kufanya miamala ya biashara husika mtandaoni kwa haraka, usafirishaji wa bidhaa hadi kwa wateja umekuwa ukikumbwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa anuani za makazi. “Mara nyingi tunajitahidi kupata taarifa za msingi alipo mteja jinsi iwezekanavyo, mara nyingi tunaangalia mwanzo wa mtaa au kituo cha basi.

Ila tunategemea sana kampuni bora za usafirishaji kukamilisha zoezi hilo ambazo huwapigia wateja na kuwapelekea wateja bidhaa ndani ya muda unaotakiwa,” anasema Mkuu wa masoko na uhusiano wa Kampuni ya Kaymu, Angaza Nkurlu.

Hata hivyo, gharama za usafirishaji zinatofautiana kutokana umbali na ukubwa unaosafirishwa, kwa Kaymu bei hizo ni kati ya Sh3,000 hadi 4,000 kwa bidhaa ndogo ndogo na umbali wa kawaida wakati Hellofood ni kati ya Sh2, 000 hadi Sh3, 000.

Mustakabali wa biashara

Mtaalamu wa Tehama, Jumanne Mtambalike anasema biashara hiyo inakuwa kwa kasi huku kampuni za kimataifa kama Kaymu na Jumia zikibisha hodi nchini na kampuni za kizawa za Kivuko, Online Shopping na Gateway na nyingine nazo zimeonyesha ushindani mkubwa. “Unajua kati ya mwaka 2011 hadi 201,3 biashara za aina hiyo zilikuwa zinafanyika kupitia mitandao ya kijamii kama Facebook kwa muuzaji kuweka bidhaa anayouza kwenye ukurasa wake au wa kundi na kuweka mawasiliano ili wateja wanaohitaji wamtafute.

“Lakini mwaka huu tumeshuhudia tovuti lukuki maalumu kwa biashara hiyo na kwa taarifa nilizopatiwa hivi karibuni, mtandao wa Kaymu Tanzania unafanya biashara na watu zaidi ya 1,000,” anasema.

Licha ya biashara hiyo kukua kwa kasi nchini, baadhi ya wananchi kama Thabiti Ibrahimu hana uhakika kwamba ununuaji wa bidhaa mtandaoni una usalama wa kutosha hususan kwenye malipo.

Matukio ya wizi wa mtandao kupitia mashine za kutolea fedha au fedha kupitia njia ya simu, anasema yanazidi kumpa hofu iwapo kweli atapata bidhaa yake ikiwa salama.

Hata hivyo, Mtambalike anasema ni lazima wengi wapate hofu kutokana kutomjua mtu anayewauzia, huku akiwatoa wasiwasi katika upande wa malipo kwa kuwa maduka mengi yanataka ulipe wakati unapokea bidhaa hivyo unaweza kuikataa iwapo umeletewa usiyoihitaji.

“Kwangu mimi vikwazo vikubwa ni vitatu: uelewa mdogo wa watu kuhusu biashara za mitandao, ukosefu wa mfumo ulio imara wa malipo na wenye ulinzi wa kutosha na usalama wa taarifa za mnunuzi na ukosefu wa mtandao baadhi ya maeneo ya Tanzania,” anasema mtaalamu huyo.

Kwa Nkurlu, changamoto zilizopo ni fursa yao kuwekeza zaidi kwa kutoa elimu kwa wananchi namna ya kununua na kuendelea kupeana utalaamu kati ya wasafirishaji na watoaji huduma kifedha ili kuboresha zaidi biashara hiyo.

0 Comments

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ZINAZOHUSIANA