Nyingine

Bajeti ya upinzani !! Wamwachia ngariba afanye anavyotaka.

Waziri kivuli wa ofisi hiyo anayeshughulikia Muungano, Ally Salehe

Mgogoro wa CUF na suala la uchaguzi wa Zanzibar jana viliibua mtafaruku bungeni baada ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kulazimishwa kuyaondoa maelezo yake kwenye hotuba yake kuhusu Bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais.

Waziri kivuli wa ofisi hiyo anayeshughulikia Muungano, Ally Salehe alisusa kusoma hotuba yake ya upinzani ya kurasa 59, kuhusu Bejeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais, baada ya kulazimishwa kuhariri maneno hayo na mengine yaliyoelezwa si ya kibunge.

Hatua hiyo ilichukuliwa na Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Zungu baada ya kusikiliza maombi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju aliyetaka maneno hayo yaondolewe.

Masaju alianza kusimama kuomba mwongozo chini ya kanuni ya 64, pale Salehe alipofika ukurasa wa pili wa hotuba yake akizungumzia fedha kidogo zinazotolewa na Serikali badala ya zilizoidhinishwa na Bunge akitumia maneno,

“Kila Wizara imekiona cha moto, maana wamebanwa mpaka wamevunjika mbavu.”

Masaju alisema maneno hayo si ya kweli kwa kuwa hakuna waziri aliyebanwa na kuvunjika mbavu.

Baada ya kauli hiyo, alisimama Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee na kufafanua kuwa ni sahihi kusema wamebanwa mbavu kwa kuwa, ni ukweli kwamba fedha zilizotolewa kwa ajili ya maendeleo ni pungufu ya asilimia 26 na kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais imepewa chini ya asilimia mbili.

SOMA NA HII:  Idara ya Habari (MAELEZO) Yapokea Msaada wa Vifaa Kutoka Ubalozi wa China

Pamoja na ufafanuzi huo, Mwenyekiti Zungu alitoa uamuzi kuwa maneno hayo si ya kibunge yafutwe na yasiingie kwenye kumbukumbu za Bunge.

Kama haitoshi, Salehe alipofika ukurasa wa tatu, aliibua songombingo nyingine, pale aliposema “Ofisi ya Makamu wa Rais imekuwa mhanga (muathirika) mkubwa wa kisu cha ngariba” kwa bajeti yake kufyekwa na kutengewa fedha ambazo hazilingani na hadhi yake.

AG Masaju aliibuka tena akitaka maneno kisu cha ngariba yafutwe kwa madai kuwa si ya kibunge na kuwa fedha hazitengwi kwa kisu na wala katika mgawo wa bajeti hakuna ukeketaji na kuhoji ni nani ambaye ni ngariba.

“Salehe unaweza kuendelea ukurasa wa nane kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu,” alisema Zungu.

Licha ya kupewa fursa ya kuendelea Salehe alisema hata hayo mengine asingeyasoma na anamwachia ngariba afanye anavyotaka.

Zinazohusiana

TOA MAONI

Kumbuka Ni Muhimu Kuandika Jina Lako