Sambaza:

Sheria ya Takwimu Na. 9 ya mwaka 2015 imeanza kutumika rasmi tarehe 2 Novemba, 2015 kupitia Tangazo la Serikali Na. 491 la tarehe 30 Oktoba, 2015.

Sheria ya Takwimu ya Mwaka 2015 haina lengo la kuzuia taasisi au watu binafsi kufanya utafiti wao nchini ila inalenga kuweka misingi imara ya shughuli za takwimu na utafiti” – Kwa mujibu wa mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Dk. Albina Chuwa.

Sheria hii hailengi kuondoa uhuru wa taasisi nyingine za utafiti kufanya kazi zao, taasisi zote za utafiti zinazotambulika katika sheria zitaendelea kuwa huru katika kufanya utafiti kwa mujibu wa taratibu zao mradi tu zinafuata sheria iliyopo.

Sheria imeanisha kuwa takwimu rasmi ni zile zitakazotolewa na Serikali kwa maana Wizara, Idara na taasisi zake kulingana na vigezo vilivyowekwa na kamisheni ya Umoja wa Mataifa ya Takwimu ambayo inatoa msisitizo wa takwimu zinazotolewa na taasisi au mtu binafsi kutambuliwa.

Sheria hii ina karibu vifungu 40, lakini kifungu muhimu zaidi ni kile cha 37 ambacho kinaweka makosa na adhabu zinazohusiana na uchapishaji wa takwimu ambazo siyo za, au hazijaidhinishwa na, Ofisi ya Taifa ya Takwimu.

Kwanza, kifungu cha 37(1)(b) kinasema kuwa mtu yeyote ambaye bila ya mamlaka halali, atachapisha au kutoa kwa mtu mwingine yeyote taarifa alizozipata kwa mujibu wa kazi yake kinyume na utaratibu wa kawaida wa ajira atakuwa ametenda kosa na akipatikana na hatia atahukumiwa faini isiyopungua milioni mbili au kifungo cha muda usiopungua miezi sita, au vyote kwa pamoja.

SOMA NA HII:  Mwongozo wa matumizi bora, sahihi na salama ya vifaa na mifumo ya TEHAMA serikalini

Pili, kifungu cha 37(1)(c) kinasema kuwa mtu yeyote ambaye anatelekeza jukumu lake au kwa makusudi atatoa tamko lolote, kauli au rejesho katika utekelezaji wa kazi yake, au anakusanya na kuzitoa taarifa zozote za uongo za takwimu atakuwa ametenda kosa na akipatikana na hatia atahukumiwa faini isiyopungua milioni mbili au kifungo cha muda usiopungua miezi sita, au vyote kwa pamoja.

Tatu, kifungu cha 37(2) kinasema kuwa mtu yeyote ambaye anamiliki taarifa yoyote ya kitakwimu, ambayo kwa ufahamu wake anajua zimetolewa kinyume na masharti ya sheria hii, anachapisha au anasambaza kwa watu wengine taarifa hizo, anatenda kosa, na akipatikana na hatia atahukumiwa faini isiyopungua shilingi milioni tano au kifungo cha muda usiopungua miezi kumi na mbili, au vyote kwa pamoja.

Nne, Kifungu cha 37(4) kinasema kuwa chombo chochote cha habari ambacho kitachapisha taarifa za kitakwimu za uongo au za upotoshaji, au kutangaza kipindi chochote kinachohusu shughuli za ukusanywaji wa taarifa ambayo imefanywa au inafanywa na Ofisi, na hatimaye kusababisha wananchi wasishiriki kwenye shughuli hiyo ya ukusanywaji wa taarifa au wasishirikiane na maafisa wa Ofisi, kinatenda kosa na kitakapotiwa hatiani kitawajibika kulipa faini isiyopungua shilingi milioni kumi au kifungo cha muda usiopungua miezi kumi na mbili au vyote
viwili.

Tano, Kifungu cha 37(5) kinasema kuwa mtu yeyote au wakala ambaye, bila idhini ya kisheria kutoka kwa Ofisi, atachapisha au kusambaza taarifa za kitakwimu ambazo zinaweza kusababisha upotoshwaji wa taarifa husika, atakuwa ametenda kosa na akipatikana na hatia atatakiwa kulipa faini isiyopungua shilingi milioni kumi au kifungo cha muda usiopungua miaka miezi ishirini na nne.

SOMA NA HII:  Selfie yamsababishia Mwanamke kifo….Akifurahia maisha.

Mwisho, kifungu cha 37(6) kinasema kuwa kwa madhumuni ya kifungu chote cha 37, “chombo cha habari” kinajumuisha kituo cha radio, kituo cha televisheni, gazeti au jarida, tovuti au chombo kingine chochote cha habari.

Sheria hii inalenga kutoa mwongozo kwa taasisi za Serikali na mashirika mbalimbali yanayotoa takwimu nchini yaweze kuendesha shughuli za ukusanyaji na usambazaji wa takwimu kwa kuzingatia sheria hiyo mpya.

Hata hivyo, inadaiwa kuwa sheria hii imeenda mbali mno kiasi cha inaweza kuifanya Tanzania kuwa mahali pagumu kwa mashirika ya uchapishaji, watafiti na wasomi kufanya kazi kwa sababu sheria hii inadhibiti uchapishaji wa takwimu zozote isipokuwa zile ambazo zimechapishwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa kuweka adhabu kali kwa yoyote yule atakayeenda kinyume na sheria hii.

Isome sheria yenyewe hapa


Sambaza:

Written by Mediahuru

Tunaandika kuhusu sayansi na teknolojia kwa kutumia lugha ya Kiswahili.

Leave a Comment

Kumbuka Ni Muhimu Kuandika Jina Lako